‘Kanisa la Mungu halimtegemei mtu fulani’ Ask. Dkt. Fredrick Shoo
- Mch. Josefu Mustafa Munisi astaafishwa kwa heshima, awahimiza wachungaji kusimama imara
- Miaka 60 ya KKKT yaadhimishwa Kidayosisi – Mungushi
- Askofu Dkt. Shoo Awaonya wanaojiinua wakidhani pasipo wao Kanisa haliwezi kusonga Mbele
Jerome Kileo, mawasiliano@northerndiocese.co.tz
Mungushi. Mkuu wa KKKT na pia KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo aliwaongoza mamia ya Washarika wa usharika wa Mungushi na wageni mbalimbali katika ibada ya Jumapili iliyoambatana na matukio makuu mawili katika Usharika wa Mungushi Jimbo la Hai la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Juni 18, 2023. Katika kuongoza ibada hiyo, Mkuu wa Kanisa na pia Dayosisi ya Kaskazini alishirikiana na Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya, Mkuu wa jimbo la Hai Mch. Biniel Malya, Mkuu wa Jimbo la Siha Mch. Elisa Kileo, Mkuu wa Pili wa Jimbo la Hai Mch. Dominick Mushi na Mch. Kiongozi wa Usharika wa Mungushi Mch. Julius Lema.
Katika ibada hiyo, Mkuu wa KKKT na pia DK, alimstaafisha kwa heshima Mch. Joseph Mustafa Munisi baada ya kutumika kama Mchungaji katika Dayosisi ya Kaskazini kwa muda wa miaka 31. Akiwa amesindikizwa na mkewe Bibi. Kwini Munisi na wanafamilia wengine, Mch. Munisi alionekana mwenye furaha na uchangamfu mwingi.
Ibada hiyo pia ilikuwa ni maadhimisho ya Kidayosisi ya Miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania tangu kuundwa kwake miaka 60 iliyopita. Akieleza hili, Mkuu wa KKKT na pia KKKT DK Ask. Dkt. Fredrick Shoo alikumbusha kwamba, KKKT iliundwa rasmi tarehe 19 Juni, 1963 huko Dar es salaam ikiwa ni matokeo ya kuunganika kwa makanisa saba (7) ambayo ni Kanisa la Kilutheri la Iraqw, Kanisa la Kiinjili la Tanganyika ya Kaskazini-Magharibi, Kanisa la Kilutheri la Tanganyika ya Kaskazini (Dayosisi yetu ya Kaskazini), Kanisa la Kilutheri la Tanganyika ya Kusini, Kanisa la Kilutheri la Tanganyika ya Kati, Kanisa la Kilutheri la Usambara-Digo na Kanisa la Kilutheri la Uzaramo-Uluguru. Kufuatia kuungana huku, Makanisa hayo yalibadilika na kuwa Kanisa Moja lililoitwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Tanganyika [sasa Tanzania] na Makanisa yaliyoungana kubadilika na kuwa Sinodi/Dayosisi na Mkutano Mkuu wa kwanza wa Kanisa Moja la Kiinjili la Kilutheri la Tanganyika ulifanyika huko Mwika mnamo tarehe 21-25 Juni, 1964 ukihusisha wajumbe kutoka Sinodi/Dayosisi zote.
Akihubiri katika Ibada hiyo, Askofu Dkt. Shoo aliwataka Wakristo kuacha kujiinua katika makanisa wanayosali na kujiona wao ndio wanaweza kusimama na kuliendesha Kanisa akisema, “Kuna watu ama walei ama watumishi wa Kanisa wanojidanganya kwamba pasipo wao Kanisa litaanguka au halitasonga mbele wakisahau kuwa Kanisa ni la Mungu. Halli hii ni ya hatari na watu wa jinsi hii wanajidanganya. Tunapaswa kufahamu kuwa Kanisa siyo muumini au waumini fulani tu, wala siyo Askofu na wachungaji au wainjilisti tu, bali ni la washarika wote kwa kuwa Kunisa ni mwili wa Kristo.” Alisema Askofu Shoo.
Aliendelea kusema kuwa, “Pia wapo baadhi ya watu wenye vipawa na karama za aina mbalimbali walizopewa na Mungu katika sharika na Kanisa lakini wanaweza kuamua kuzira na kukaa pembeni kwa sababu tu labda mchungaji hajaendana na matakwa yao. Watu kama hawa ni sawa na nyani anayeamua kuziria mti; sasa sijui wakati wa hatari atakimbilia wapi; kuziria kazi ya Kanisa ni Kumziria Mungu ambaye ndiye aliyekupa vitu vyote; mali, karama, uhai n.k.” Alieleza Askofu Dkt. Shoo.
Aidha, alimshukuru Mungu kwa maisha ya utumishi ya mchungaji Joseph Mustafa Munisi na kumtakia baraka yeye na familia yake. Pia aliwashukuru washarika wa Mungushi kwa kuandaa tukio la kumstaafisha Mch. Munisi pamoja na maadhimisho ya Miaka 60 ya KKKT.
Akizungumza wakati wa kutoa neno la itikio punde baada ya kustaafishwa kwa heshima; Mch. Joseph Musta Munisi (mstaafu) alimshukuru Mungu kwa kumpa kibali cha kutumika katika shamba la Bwana na hadi kufikia siku ya kustaafu kwake kwa heshima. Pia alilishukuru kanisa na viongozi kwa kumuita kutumika katika shamba la Bwana. Alisema kuwa wakati alipokuwa akitaka kuanza huduma hiyo ya kichungaji alikutana na changamoto nyingi ikiwemo ya kuatishwa tamaaa ya kufanya huduma hiyo lakini aliamuaa kumtegemea Mungu na Mungu alimvusha na kuweza kufanya kazi hiyo ya Mungu mpaka kufikia kustaafu kwake. Mch. Munisi (mstaafu) alihitimisha itikio lake kwa kuwarai watumishi wenzake walioko kazini kuendelea kusimama imara na kukabiliana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika dunia wakitambua kuwa Yesu Kristo anapenda wawalete watu wake kwake [Yesu] na siyo kwao [wachungaji/wainjilisti], kama wafanyavyo wale wajiitao mitume na manabii, hivyo aliwahimiza waendelee kutumika kwa uaminifu na kikamilifu.
Kwa upande wake, Mchungaji Kiongozi wa Usharika huo wa Mungushi Mch. Julius Lema alisema kuwa katika miaka 60 ya KKKT, Kanisa linaendelea kuwa lenye kuaminika katika jamii na hivyo, kila mara ni muhimu kwa kila mmoja wetu kumshukuru Mungu kwa umoja na kuaminika kwa KKKT. Kabla ya kufunga ibada, Mkuu wa KKKT na pia KKKT DK Ask. Dkt. Shoo alirudia tena kumshukuru Mch. Kiongozi, baraza la usharika na washarika wa Mungushi kwa ukarimu wao na moyo wa upendo katika kufanikisha ibada ya kumstaafisha Mch. Munisi kadhalika maadhimisho ya miaka 60 ya KKKT, aliwatakia baraka tele huku akitumia maneno ya bashasha ya lugha ya Kimachame “aikany mnu nde na ma” kwa Kiswahili cha moja kwa moja “asanteni sana mabwana na mabibi”!
