Prof. Maanga Astaafu kwa Heshima

Mhe. Baba Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo ameongoza ibada ya kumstaafisha kwa heshima Mchungaji Profesa Godson Solomon Maanga katika Usharika wa Lole Juni 25, 2022.

Kabla ya kuanza kwa ibada hiyo, Askofu Dkt. Shoo alifungua jengo la ukumbi wa mikutano na jiko la Usharika lililogharimu  shilingi milioni 47.

Katika Ibada hiyo Askofu Dkt. Shoo alihubiri juu ya Safari ya Kwenda Mbinguni. Alisema wito wa kwenda  Mbinguni umewekwa na Yesu Kristo kwa kuja kwake duniani, kufa kwa ajili yetu na kufufuka kwake.

Alisema japo safari hiyo ni ngumu yenye dhiki na taabu nyingi tusisahau kumtanguliza Yesu Kristo ambaye kwa kufa kwake na kufufuka  na pale tutakapo mwamini na kumtegemea atatufikisha kwa baba pale alipotuandalia makao ya milele.

Alisistiza hakuna sababu ya kukata tamaa katika safari yetu ya  kwenda  Mbinguni japo ni yenye dhiki na majaribu. Alisema hata Yesu alisema duniani kunayo dhiki lakini jipeni moyo mtashinda

Kwenda mbinguni si kama kwenda langoyo (sokoni}, wito wa kuingia mbinguni unamaanisha kuwa mvumilivu”Alinukuliwa Dkt Shoo.

Awali alimpongeza Mchungaji Profesa Mahanga katika utumishi wake wa muda mrefu katika Kanisa na Dayosisi akitumia vipawa mbalimbali alivyopewa na Mungu.

Akisoma historia ya utumishi wake Katibu Mkuu wa Dayosisi Mhandisi  Z.S.Moshi, alisema historia ya Mch. Prof. Maanga ina mambo mengi muhimu ya kujifunza.

“Historia ya Mch. Prof. Maanga ina mengi muhimu na ni ndefu sana kama kurasa 30, kwa idhini yake nitasoma muhtasari wa kurasa 5, Dayosisi ina enzi watu kama yeye n.k. hivyo historia yake itahifadhiwa katika Makavazi (Archive) ya Dayosisi alisema Mhandisi Z.S.Moshi.

Mch. Prof. Maanga alizaliwa 1955, alibarikiwa kuwa Mchungaji Disemba 6, 1981 katika Usharika wa Kotela Mamba. Amekuwa Mchungaji kiongozi katika sharika za Kotela, Ivaeny na Kondeny.

Pia katika utumishi wake wa takribani miaka 40 amefundisha katika Chuo cha Biblia Mwika, Mhadhiri  Chuo cha Tumaini Makumira, Mkuu wa Chuo cha Bibilia na Theolojia Mwika na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCo).

Akitoa neno la itikio Mch. Prof. Maanga aliwaasa wachungaji waliopo kazini kuhubiri kweli ya neno la Mungu na kusimama katika haki siku zote.

“Mwisho wa mechi ni muhimu kuliko mwanzo wa mechi kwa sababu kipenga cha mwisho ndicho huamua matokeo, zingatieni sana kudumu katika wito wenu wa kichungaji hadi mwisho”. Mch. Prof, Maanga alisema akihitimisha neno lake la itikio.

Askofu Dkt. Fredrick Shoo akikata utepe wakati akizindua jengo la ukumbi wa Mikutano na Jiko la Usharika wa Lole Juni 25,2022