Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo aliongoza kikao cha Wanadayosisi waliopo Safarini (Diaspora) Disemba 27, 2023 Uhuru Lutheran Hotel& Conference Centre kikao ambacho hufanyika kila mwisho wa mwaka kujadili masuala mbalimbali yahusuyo maendeleo ya Dayosisi.

Sambamba na kikao hicho, alizindua rasmi gazeti la kila wiki la Umoja Daima ambalo awali lilikuwa likitoka kama Jarida kila baada ya miezi mitatu.

Akizungumza katika kikao hicho Askofu Dkt. Shoo amewataka wakristo waishio nje ya Dayosisi kujitoa katika kuboresha taasisi mbalimbali za kimaendeleo zilizopo katika Dayosisi.

Alisema kuwa michango na ushauri unaotolewa na wanadayosisi waliopo safarini inasaidia katika kuendeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kwamba ushauri wao umekuwa ukifanyiwa kazi katika kuboresha taasisi zilizopo.

Aidha aliwapongeza wanadayosisi walioko safarini kwani wamekuwa mfano mwema katika maeneo wanayoishi kwa kufanya kazi nzuri na kuwaeleza kuwa kufanya hivyo kunawaletea baraka za Mungu.

“Ninawaomba muendelea kumtumikia Mungu kwa kutoa huduma za kiroho na kimwili popote mlipo” Alisistiza Askofu Dkt. Shoo.

Kwa upande wa Wanadayosisi waliopo nje wamesema kuwa, kukutana kwao na Mkuu wa Dayosisi kumekuwa na manufaa kwani imekuwa ni sehemu mojawapo ya kupata taarifa zinazoendelea ndani ya Dayosisi yao.

Akihitimisha hotuba yake Askofu Shoo aliwataka Wanadayosisi popote watakapokuwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka 2024.