Usharika wa Bonite wazinduliwa rasmi

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, amezindua rasmi Usharika mpya wa Bonite uliopo Jimbo la Kilimanjaro Kati Oktoba 31, 2021. Uzinduzi huo uliambatana na tendo la kuwabariki wanafunzi wa Kipaimara 47 na kuwapa vyeti wahitimu 22 wa Elimu ya Theologia Enezi (ETE)

Akihubiri katika ibada hiyo Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya aliwataka wachungaji kufundisha kweli ya neno la Mungu kama Martin Luther na nabii Habakuki walivyofanya. “Tufundishe kweli ya neno la Mungu, washarika turudi tusome neno la Mungu na kulitafakari ili tusipotoshwe na mafundisho ya uwongo.

Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi mchungaji kiongozi wa Usharika huo Mch. David Palango amesema  historia ya usharika mpya wa Bonite ni muendelezo wa historia ya uliokuwa usharika wa Kiyungi ambao kwa sasa  hautambuliki tena kwa jina hilo.

Usharika wa Kiyungi sasa Bonite ni miongoni mwa sharika zilizotokana na uliokuwa usharika wa Chemchem na Arusha chini ambao ulizinduliwa rasmi Januari Mosi, 1993. Usharika wa Kiyungi ulianza na washarika 883 idadi ambayo imeendelea kukua na sasa usharika mpya wa Bonite unawasharika 900.