Wanafunzi 249 wa kozi ya Elimu ya Theolojia Enezi (ETE) wamehitimu masomo yao katika ngazi ya kati na kutunukiwa vyeti na Mkuu wa KKKT ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Baba Askofu Dkt.Fredrick Onaeli Shoo, kwenye ibada iliyofanyika katika Usharika wa Moshi mjini Mei 2, 2021.
Baba Askofu aliwahitimisha wahitimu hao kutoka katika sharika mbalimbali za Dayosisi ya Kaskazini baada ya kufuzu kozi hiyo ya miezi tisa.
Kozi hiyo hufundishwa kwenye vituo mbalimbali vya mafunzo katika majimbo kuwawezesha kutoa elimu ya Kikristo katika shule,vyuo na jamii kwa ujumla.
Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mch. Elingaya Saria (mstaafu) akihubiri katika ibada hiyo aliwataka, Wakristo kumsifu na kumtukuza Mungu kwa kumwimbia nyimbo za sifa.
Ikiwa ni Jumapili ya Kantante Domino, maalumu kwa ajiliya kumwimbia na kumsifu Mungu aliye hai alisema, mwanadamu ana kila sababu ya kumsifu na kumtukuza Mungu siku zote.
”Kila mwenye pumzi ana kila sababu ya kumtukuza na kumsifu Mungu, hata viumbe vinamsifu na kumtukuza Mungu, tukitazama uumbaji wa Mungu,sayari, jua, upepo, bahari, mito, na vyote alivyoviumba na jinsi vilivyo katika utaratibu wa kupendeza tunasema tuna kila sababu ya kumsifu na kumtukuza Mungu.”Alisema Mch.Saria
Alisema hata Musa aliwambia wana Waisraeli wamsifu Mungu na kumtukuza, baada ya Mungu kuwatoa utumwani Misri na kuwavusha katika bahari ya Shamu kuelekea nchi ya ahadi.
Aidha aliwapongeza wahitimu hao wa ETE Kwa kuhitimu mafunzo yao na kuwatakia baraka katika kuifanya kazi ya Mungu. “Kwanza nafarijika kuona idadi kubwa ya wahitimu hawa wote 249, mtakua baraka na msaada katika kutoa Elimu ya Kikristo kwani kuna uhitaji mkubwa katika jamii.”Alisema Mch. Saria
Naye Mkuu wa Kanisa na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini aliwataka wahitimu hao kuitumia vyema elimu waliyopata katika kuhudumia jamii na kutoa wito kwa sharika kuendelea kutuma wanafunzi kwa ajili ya kupata mafunzo hayo kwani kuna uhitaji mkubwa.
“Kuna uhitaji mkubwa wa watu wenye elimu ya Theologia kusaidia katika shule za jumapili, ibada za nyumba kwa nyumba, shule, vyuoni na katika jamii” Alisema Askofu Dkt.Shoo.
