Mahafali ya nane ya Wanafunzi wa darasa la saba wa Shule ya Msingi kwa Watoto wenye Ulemavu wa Viungo Faraja Maalum yamefanyika Oktoba 8, 2022 katika shule ya msingi Faraja Maalum katika jimbo la Siha la KKKT Dayosisi ya Kaskazini.
Katika mahafali hayo jumla ya wanafunzi 26 wamehitimu masomo yao baada ya kufanya mtihani wa taifa wa darasa la saba uliofanyika Oktoba 6 na 7, 2022.
Sambamba na mahafali hayo, Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya kabla ya kuanza kwa mahafali hayo alifungua Bwalo liliojengwa kwa takribani zaidi ya shilingi milioni 380 pamoja na Karakana ya mafunzo kwa vitendo katika kada ya ushonaji, uchomeaji na useremala yenye thamani ya shilingi milioni 20.
Akizungumza kwenye mhafali hayo, Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya amewapongeza wahitimu kwa kumaliza elimu yao ya msingi pamoja na uongozi kwa kazi nzuri wanayoifanya shuleni hapo.
Alitoa wito kwa jamii kutoa habari njema ya huduma inayotolewa shuleni hapo kusaidia wazazi na walezi kuwatoa watoto wao na kuja kuhudumiwa.
“Naombeni kila mmoja wetu akatoe habari njema ya huduma hii, tukitoa habari nzuri za hapa Faraja tutatatua changamoto ya wale wazazi na walezi wanaowafungia ndani watoto wenye welevu”
Pia Mch. Msanya aliishukuru Serekali kwa mchango wake na kuiomba Serekali kuongeza nguvu zaidi ili huduma zinazotolewa zifanyike kwa ufanisi zaidi.
“Naishukuru Serekali kwa mchango wake; tumesikia Serikali yetu inachangia asilimia 11 niombe waongeze nguvu zaidi ili huduma iendelee kutolewa kwa ufanisi zaidi”
Naye mwenyekiti wa Faraja Fund Foundation Bw. Dave Tolmie aliwapongeza wahitimu hao na kuahidi kuendelea kuwafadhili katika masomo yao ya juu.
Kwa upande wa wahitimu katika risala yao walieleza mafanikio waliyopata shuleni hapo kuwa ni pamoja na ujuzi na maarifa, mafunzo ya computer, matibabu ya viungo na kutengamaa kwa viungo.
Shule ya Msingi Faraja Maalum inamilikiwa na KKKT Dayosisi ya Kaskazini. Ina jumla ya wanafunzi 92 ambapo inauwezo wa kupokea jumla ya wanafunzi 100 kwa madarasa yote.
Aidha katika risala hiyo walitaja pia changamoto zinazowakabili kuwa ni mapungufu ya vitabu vya kiada, Gari aina ya Costa kwa ajili ya safari hususani za matibabu, upungufu wa vyumba vya madarasa ambapo mgeni rasmi Mhe. Msaidizi wa Askofu Mch. Msanya aliiomba bodi ya shule kuainisha changamoto hizo na kuziwasilisha sehemu husika.