“ninakumbuka wakati wa ujana wangu, nililazimika kuchagua kusoma shule ya karibu na nyumbani, ili tu niweze kuwaangalia na kuwatunza bibi na babu wangu…” ashuhudia mshiriki mmojawapo. Nukuu hii siyo ya moja kwa moja.
Hiyo na masuala mengine mengi, yalikuwa sehemu ya hotuba, mada, majadiliano na ushuhuda muhimu katika semina ya Utunzaji wa Wazee iliyoandaliwa na KKKT Dayosisi ya Kaskazini siku ya Jumatano tarehe 12 Septemba, 2023 katika ukumbi wa Umoja Hall, Lutheran Umoja Hostel.
Akifungua semina hiyo, Mhe. Msd. Ask. Mch. Deogratius Msanya alisema, “lengo la semina hii ni kuona ni kwa jinsi gani KKKT Dayosisi ya Kaskazini, inaweza kushiriki kwa namna bora kabisa katika Mpango wa Taifa wa Huduma ya Afya Bora kwa wazee. Hii ni pamoja na kuhakikisha kunakuwepo na mpango na mwongozo thabiti wa utunzaji wa Afya ya wazee katika ngazi zote Dayosisi kuanzia jumuiya, mitaa, sharika, majimbo na Dayosisi”.
Naye mwezeshaji mkuu wa semina hiyo Dkt. Elihuruma Nangawe pamoja na mambo mengine mengi, alisisitiza kuhusu;
- Umuhimu wa jamii kwa ujumla kuelewa wajibu na majukumu ya mtu mmojammoja, jumuiya, mitaa, sharika, majimbo, Dayosisi na Kanisa kwa ujumla ili kupata ufanisi wa utekelezaji wa Mpango wa huduma ya Afya Bora kwa wazee iliyopo kwenye mpango wa Taifa.
- Umuhimu na ulazima wa jamii, hususan wazee wenyewe kujengewa uwezo wa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha na kufuatilia utekelezaji wa mpango huo katika ngazi zote za Dayosisi na Kanisa kwa ujumla.
- Umuhimu na ulazima wa wazee wenyewe kuzingatia mambo kadhaa yahusuyo afya zao k.v. kufanya mazoezi mepesi yanayojumuisha kutembea, kujinyoosha n.k, kuwa waangalifu katika vyakula n.k.
- Jamii kwa ujumla wake, kuona wajibu muhimu wa kuwaepusha wazee na upweke kwa kuwatembelea au kuwajengea vikundi vya kutembeleana katika jumuiya na hata kuwawezesha kutumia TEHAMA k.v. mitandao ya kijamii n.k.
Katika semina hiyo, washiriki walipata fursa ya kuuliza maswali, kufanya majadiliano katika vikundi na hata kutoa ushuhuda binafsi wa maisha yao kama wanafamilia waliotunza wazee na pia kama wazee. Katika ushuhuda mmojawapo, mshiriki mmojawapo aliisisimua hadhira aliposhuhudia kwamba, “ninakumbuka wakati wa ujana wangu, nililazimika kuchagua kusoma shule ya karibu na nyumbani, ili tu niweze kuwaangalia na kuwatunza bibi na babu wangu…”
Mpendwa rafiki unayetembelea mtandao wa kijamii wetu, tunapenda utushirikishe;
- Unachofahamu kuhusu Mpango wa Taifa wa Huduma ya Afya Bora kwa wazee.
- Maoni yako kuhusu njia yenye ufanisi zaidi ya kuwatunza wazee wetu.