ZIARA YA ASKOFU SHOO USHARIKA WA LOWASI YALETA FURAHA

Ni furaha, shangwe na shukurani katika Mitaa ya Usharika wa Lowasi Jimbo la Kilimanjaro Kati KKKT Dayosisi ya Kaskazini, ambapo uwekaji wa mawe ya msingi na ufunguzi wa miradi mbalimbali umefanyika.

Matukio hayo yameongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Dkt. Fredrick Shoo, ambae alianza katika mtaa wa Sasaya katika uwekaji wa jiwe la Pembe katika jengo la Darasa la Chekechea na Jiko.

Akiwa hapo Askofu Shoo amewapongeza washarika wa mtaa huo kwa kukumbuka kujenga eneo maalumu kwa ajili ya Watoto.

Katika mtaa wa Lowasi ambako ni senta ya Usharika huo, kumekuwa na ufunguzi wa jengo lililokamilika ambalo ni Jiko na ukumbi pamoja na Jenereta la kuzalisha nishati ambalo lilinunuliwa kwa michango ya washarika na marafiki wa mtaa huo.

Baada ya  mtaa wa Lowasi Askofu Shoo aliekea mtaa wa Kyele, ambako aliweka Jiwe la Pembe la ujenzi wa Jengo la kanisa na kuzindua rasmi harambee ya ujenzi inayotarajiwa kufanyika mwezi Disemba mwaka huu.

Katika mahubiri yake Askofu Shoo amesema Kanisa la Mungu mahali popote lilipo linapaswa kugusa hali na mapito ya watu wake,na si kwa kutambua changamoto zao pekee, bali kwa kuingia katika mioyo yao na kuwagusa kiroho kwa kuwaombea.

Aidha kwa mujibu wa risala iliyowasilishwa katika ibada hiyo, wazo la kuanzisha Mtaa wa Kyele lilianza mwaka 2016 kwa lengo la kupunguza umbali wa waumini kwenda katika nyumba ya ibada iliyopo mtaa Lowasi. Risala hiyo imeelekeza ombi kwa Baba Askofu kuwajulisha marafiki mbalimbali watakaowawezesha kufanikisha harambee ya ujenzi wa jengo hilo.

Askofu Shoo amewasisitiza washarika wa Lowasi na hasa mtaa wa Kyele, kutokata tamaa kwa kazi ya ujenzi iliyopo mbele yao, bali wazidi kuwa na umoja na kuamini kuwa Bwana Mungu atawafanikisha