MCH. JOYCELINE NJAMA ASTAAFU BAADA YA MIAKA 40 YA UTUMISHI, ASKOFU SHOO ASISITIZA UMUHIMU WA UVUMILIVU

Mchungaji Joyceline Njama amestaafu rasmi baada ya kulitumikia Kanisa kwa miaka 40. Ameastaafishwa na Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, katika ibada iliyofanyika Novemba 8, 2026, katika Kanisa Dogo la Hagai Chapel, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro (KCMC).

Akihubiri katika ibada hiyo, Askofu Shoo amesisitiza umuhimu wa uvumilivu katika maisha ya Kikristo, akieleza kuwa kumfuata na kumtumikia Kristo kunahitaji imani na uvumilivu wa kudumu licha ya changamoto, upinzani na majaribu yanayoweza kujitokeza.

Amesema hata Kanisa la mwanzo lilipitia mateso na changamoto mbalimbali, lakini liliendelea kusimama kutokana na uvumilivu wa waumini. Aidha, ameitaka jamii kujenga utamaduni wa kuvumiliana, kufanya kazi kwa bidii na kujitoa katika kutimiza majukumu yake.

Kwa upande wake, Mchungaji Mstaafu Joyceline Njama amesema safari yake ya kuingia katika masomo ya Theolojia haikuwa rahisi, hasa kwa wanawake wa mwanzo waliojiunga na mafunzo ya uchungaji, ambao walikumbana na mshangao na mitazamo hasi kutoka kwa baadhi ya watu. Hata hivyo, waliendelea na masomo hadi kufikia hatua ya kubarikiwa kuwa wachungaji.

Akitoa salamu za shukrani, amesema katika miaka 40 ya utumishi wake amepitia changamoto mbalimbali, lakini amezitazama kama fursa zilizomjenga na kumuimarisha katika huduma yake.

Aidha, amewataka wanafunzi na watafiti kuhakikisha matokeo ya tafiti zao yanawafikia viongozi wa Kanisa na kutumika kutatua changamoto zilizopo, badala ya kubaki kwenye makabati na mashelfu.