Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Mhe. Enock Koola, leo Septemba 28, 2026, amekabidhi hundi ya shilingi milioni 100 kwa Hospitali ya Marangu inayomilikiwa na KKKT Dayosisi ya Kaskazini, kwa ajili ya ujenzi wa kliniki ya kisasa ya kinywa na meno.
Fedha hizo, ambazo ni mchango wa Mbunge pamoja na marafiki zake, zimepokelewa na Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo mbele ya wadau, wataalamu wa afya na viongozi wa serikali.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Askofu Shoo amesema Kanisa limekuwa likifanya kazi ya kumhudumia mwanadamu katika maisha yake, huku Hospitali ya Marangu ikiwa miongoni mwa ushahidi wa huduma hiyo.
Askofu Shoo amesema Kanisa limekuwa tayari kushirikiana na Serikali katika kuwahudumia wananchi, akisisitiza umuhimu wa kutunza tunu hiyo ya ushirikiano ili isiweze kupotea.
Kwa upande wake, Mbunge Enock Koola amesema anatamani siku moja watu wanapozungumzia huduma za meno, Hospitali ya Marangu iwe miongoni mwa vituo vitakavyotajwa, jambo ambalo limemfanya kulibeba suala hilo.
Mbunge Koola amesema ataendelea kushirikiana na KKKT Dayosisi ya kaskazini katika miradi mingine, ili kuhakikisha hospitali hiyo inapata heshima sawa na uzoefu wake wa miaka mingi katika kutoa huduma.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Godfrey Mnzava, amelishukuru Kanisa kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwahudumia wananchi na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo.
Daktari Kiongozi wa Hospitali ya Marangu, Dkt. Janeth Mgonja, amewashukuru viongozi hao na kuweka wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kushiriki katika kuboresha huduma za hospitali.




