WAFADHILI WA GLOBAL HEALTH MINISTRY WATEMBELEA KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI

Wafadhili kutoka huduma ya Global Health Ministry wametembelea ofisi za Makao Makuu ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini, zilizopo Moshi Mjini, Oktoba 8, 2026, kwa lengo la kujionea na kutathmini miradi mbalimbali wanayoifadhili katika hospitali za Dayosisi hiyo.

Katika ziara hiyo, wafadhili hao wamekutana na uongozi wa Dayosisi, ukiongozwa na Askofu Dkt. Fredrick Shoo, ambapo mazungumzo yao yamejikita katika kuimarisha ushirikiano wa kuboresha huduma za afya kupitia ufadhili wa vifaa tiba kwa hospitali na vituo vya afya vya Dayosisi.

Akizungumza kuhusu ziara hiyo, Katibu wa Afya wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Bw. Joshua Ndaga, amesema lengo la ziara hiyo ni kuona na kutathmini utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Global Health Ministry katika hospitali za Dayosisi.

Amesema huduma hiyo imekuwa ikisaidia hospitali hizo kwa kutoa vifaa tiba vyenye thamani inayokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi milioni 552, hatua inayochangia kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Aidha, mazungumzo kati ya Askofu Dkt. Shoo na wafadhili hao yamekuwa fursa kwa Dayosisi kutoa shukrani kwa msaada huo na kueleza umuhimu wa vifaa tiba vilivyotolewa katika kuimarisha huduma za afya katika hospitali na vituo vyake vya afya.

Ziara hiyo ni sehemu ya ushirikiano kati ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini na Global Health Ministry unaolenga kuendeleza na kuboresha huduma za afya kupitia ufadhili wa vifaa tiba.

Katika kuhitimisha ziara hiyo, Askofu Dkt. Shoo amewakabidhi wageni hao zawadi maalumu kama ishara ya shukrani na ukumbusho wa ziara yao katika ofisi za Makao Makuu ya Dayosisi.