ELCT ND-SACCOS YATOA SHUKRANI KWA WATUMISHI WA KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI

Ujumbe wa ELCT ND-SACCOS umewasilisha shukrani kwa uongozi na watumishi wa Ofisi Kuu za KKKT Dayosisi ya Kaskazini, kutokana na namna watumishi hao wanavyotumia huduma za Saccos hiyo.

Shukrani hizo zimetolewa katika sala ya asubuhi iliyofanyika leo, Oktoba 8, 2026, ambapo ujumbe huo umeongozwa na Bw. Andrew Materu ambae ni meneja wa Saccos hiyo ambao katika tukio lililoambatana na  kuwasilisha zawadi ya keki kwa uongozi wa Dayosisi.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi na watumishi wa Ofisi Kuu za Dayosisi, Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo amepokea salamu hizo na kueleza kuwa huduma zinazotolewa na ELCT ND-SACCOS zimekuwa sehemu muhimu kwa watumishi wa ofisi hiyo.

Kwa upande wake, Bw. Andrew Materu amesema wameamua kufikisha ujumbe huo wa shukrani kutokana na namna watumishi wa Ofisi ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini wamekuwa watumiaji wazuri wa huduma zinazotolewa na ELCT ND-SACCOS.

Materu amesema hawajawahi kupata changamoto katika utoaji wa huduma kwa watumishi hao, hususan katika huduma za mikopo pamoja na urejeshaji wa mikopo hiyo.

Akizungumza baada ya kupokea ujumbe huo, Askofu Dkt. Fredrick Shoo ameonesha kufurahishwa na hatua hiyo, huku akiwahimiza watumishi kuendelea kutumia huduma za ELCT ND-SACCOS badala ya kujihusisha na mikopo yenye masharti magumu na yenye madhara kwa watumishi, maarufu kama mikopo ya “kausha damu.”