Saccos ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini (ELCT ND-Saccos) imehitimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kuwakutanisha wafanyakazi,wadau na wanachama wake kwa lengo la kuboresha mahusiano na kuendeleza ushirikiano.
Tukio hilo limefanyika leo, Oktoba 9, 2026, katika tawi la Saccos hiyo lililopo Moshi mjini, ambapo wanachama na wafanyakazi kutoka matawi mbalimbali wameshiriki kwa pamoja katika sala ya asubuhi, ikifuatiwa na tafrija fupi.
Akizungumza katika tafrija hiyo, Mwenyekiti wa ELCT ND-Saccos, Mch. Anna Makyao, amewahimiza wanachama na vijana kuwa na utaratibu wa kuweka akiba kwa ajili ya kujenga maisha bora ya baadaye.
Pia, amewahimiza kuchangamkia fursa za umiliki wa viwanja katika miradi ya Saccos hiyo iliyopo Msalato, Dodoma, na Bomang’ombe, mkoani Kilimanjaro.
Kwa upande wake, Magret Mahimbo, ambaye ni mwanachama wa Saccos hiyo, ameeleza kuwa amepata maendeleo mbalimbali ya kiuchumi kupitia mikopo na huduma za kifedha anazopata kutoka katika chama hicho.
Naye Gloria Baida, ambaye amekuwa mwanachama wa Saccos hiyo tangu akiwa binti mdogo, ameeleza kuwa mikopo ya elimu inayotolewa na chama hicho imemuwezesha kuendelea na masomo hadi kufikia ngazi ya stashahada.
Akizungumzia huduma za chama hicho, Meneja wa Miradi na Masoko wa ELCT ND-Saccos, Bw. Jeremia Chaki, amesema kuwa chama hicho kitaendelea kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wanachama na kutatua changamoto zao.




