MARAFIKI WA CHUO CHA BIBLIA MWIKA WATEMBELEA KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI, MAHUSIANO YA MIAKA 50 YAADHIMISHWA

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, amepokea ujumbe wa wageni 10 kutoka Wunsiedel na Weiden nchini Ujerumani, ambao ni marafiki wa Chuo cha Biblia na Theolojia Mwika, katika Ofisi Kuu ya Dayosisi  Oktoba 15, 2026.
Wageni hao waliwasili nchini kwa ajili ya kushiriki maadhimisho ya Jubilii ya miaka 50 ya ushirikiano kati yao na Chuo cha Biblia na Theolojia Mwika, yatakayofanyika Oktoba 24, 2026, chuoni hapo.
Akizungumza wakati wa kuwapokea wageni hao, Askofu Dkt. Shoo amesema ni furaha kubwa kuwapokea na kuwa nao nchini Tanzania, hususan katika Dayosisi ya Kaskazini. Aidha, ameeleza kuwa uhusiano huo umekuwa baraka kutoka kwa Mungu na ni sababu ya pande zote kumshukuru Mungu kwa kuwawezesha kudumisha ushirikiano huo kwa kipindi cha nusu karne.
Askofu Shoo alisisitiza kuwa mahusiano yanaweza kuanzishwa na kuvunjika ndani ya muda mfupi, lakini kudumu kwa ushirikiano huo kwa miaka 50 ni ushuhuda unaopaswa kuambatana na shukrani kwa Mungu.
Amesema kuwa pande hizo zimeendelea kutembea pamoja kwa muda mrefu kutokana na kuwa na lengo moja la huduma, ambalo ni kueneza Injili ya Yesu Kristo.
“Kwetu sote huu ni wakati wa kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kutembea pamoja kwa miaka 50. Tuna huduma moja ya kueneza Injili ya Yesu Kristo, na mahusiano haya yametupa nafasi ya kushirikiana katika utume huo,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa ziara hiyo itawawezesha kukaa pamoja, kujadiliana na kutafakari namna bora ya kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya huduma ya Kanisa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Biblia na Theolojia Mwika, Mchungaji Obed Akyoo, amesema wageni hao waliwasili nchini Oktoba 13, 2026, na wamepata fursa ya kutembelea Makao Makuu ya Dayosisi ya Kaskazini kabla ya kushiriki maadhimisho ya Jubilii ya miaka 50 ya ushirikiano wao na chuo hicho.
Naye Mchungaji Joerg Mahler kutoka Bavaria, Ujerumani, ameishukuru Dayosisi ya Kaskazini kwa mapokezi mazuri na kueleza kufurahishwa kwake na namna Kanisa linavyoendesha huduma zake nchini Tanzania.
Alisema wamevutiwa na ukarimu walioupata pamoja na idadi kubwa ya waumini wanaoshiriki ibada nchini Tanzania, akilinganisha hali hiyo na mwenendo wa Kanisa katika eneo la Bavaria, ambako, kwa maelezo yake, ushiriki wa waumini na ukuaji wa Kanisa vimekuwa changamoto.
Mchungaji Mahler ameeleza kuwa hali hiyo inawafanya kuhitaji maombi kutoka kwa Wakristo wa Tanzania ili Mungu aliimarishe Kanisa nchini Ujerumani na kulisaidia kuendelea kukua kiroho.
Ziara hiyo inaweka alama muhimu katika historia ya ushirikiano kati ya Chuo cha Biblia na Theolojia Mwika na marafiki zake kutoka Ujerumani, huku maadhimisho ya miaka 50 yakitarajiwa kuwa fursa ya kushukuru kwa safari iliyopita na kuweka msingi wa kuendeleza ushirikiano huo katika kuhubiri Injili ya Yesu Kristo.