IDARA YA AFYA KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI YAPATA GARI JIPYA, ASKOFU SHOO AZINDUA

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, Oktoba 21, 2026, ameweka wakfu gari jipya aina ya Toyota Land Cruiser lililonunuliwa kwa ajili ya Idara ya Afya – Dayosisi, kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za idara, hususan programu ya Elimu ya Afya ya Msingi.

Upatikanaji wa gari hilo unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuboresha usafiri na kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya Idara ya Afya, baada ya gari lililokuwa likitumika awali kuchakaa na hivyo kuhitaji chombo kipya cha usafiri kitakachowezesha shughuli za idara hiyo kuendelea kwa ufanisi.
Idara ya Afya ina jukumu muhimu katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala mbalimbali ya afya, kuhamasisha wananchi kuzingatia kanuni za afya na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa. Katika kutekeleza majukumu hayo, usafiri ni nyenzo muhimu inayosaidia wataalamu na waratibu kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza katika hafla ya kuweka wakfu gari hilo, Askofu Dkt. Shoo ametoa shukrani zake kwa marafiki wa Dayosisi hiyo kutoka nchini Ujerumani kwa kuendelea kuunga mkono shughuli za Elimu ya Afya ya Msingi, pamoja na mchango wao uliowezesha kupatikana kwa gari hilo jipya.
Askofu Shoo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na wadau mbalimbali katika kuendeleza huduma zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi, akitambua mchango wa marafiki hao katika kusaidia shughuli za afya zinazotekelezwa na Dayosisi ya Kaskazini.
Kwa upande wake, Mratibu wa Elimu ya Afya ya Msingi, Bibi. Isaria Megiroo, amesema kuwa kupatikana kwa gari hilo kutarahisisha kazi za idara hiyo, hasa katika kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi wakati wa kutekeleza shughuli za utoaji wa elimu ya afya.
Amesema kuwa chombo hicho kipya cha usafiri kitakuwa msaada mkubwa kwa watendaji wa programu hiyo, kwa kuwa kitawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa urahisi zaidi na kurahisisha usafiri.