KKKT Dayosisi ya Kaskazini, NCA Waandaa Mafunzo ya Vijana wa Dini Mbalimbali

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, kwa kushirikiana na Shirika la Norwegian Church Aid (NCA), limeandaa semina ya mafunzo kwa vijana kutoka dini mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kudumisha umoja, upendo na amani, pamoja na kutambua fursa za kiuchumi na kijamii zinazowazunguka. Mafunzo hayo yamefanyika, Oktoba 30, 2026, katika ukumbi wa Lutheran Uhuru Hotel, Moshi, na kuzinduliwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dkt. Fredrick Onael Shoo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Interfaith Mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Askofu Shoo amewataka vijana nchini kutokubali kugawanywa au kugombanishwa kwa misingi ya tofauti za kidini, bali waendelee kudumisha uzalendo, umoja na upendo, akisisitiza kuwa ushirikiano wao ni msingi muhimu wa kuleta maendeleo na kuimarisha mshikamano wa kitaifa. Amesema kukutana kwa vijana wenye imani tofauti na kuungana katika kuwahudumia watu kwa upendo na amani ndiko kunakodhihirisha nguvu ya ushirikiano wa dini mbalimbali (Interfaith). Pia, amepongeza uwakilishi wa vijana wa jinsia zote katika mafunzo hayo.

Aidha, amewahimiza vijana kutambua na kutumia fursa zilizopo katika mazingira yao ili kujiajiri na kujiletea maendeleo, badala ya kutegemea ajira rasmi za serikalini au katika taasisi mbalimbali. Kwa upande wake, Padre wa Kanisa Katoliki la Roma, Dkt. Aidan Msafiri, amewataka vijana kujitambua, kufikiri nje ya mazoea na kutumia fursa zinazowazunguka ili kujiletea maendeleo na kuchochea mabadiliko chanya katika jamii.

Amesema ujana ni kipindi ambacho mtu anakuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, kubuni na kutekeleza mawazo mbalimbali, hivyo ni muhimu kwa vijana kutumia nguvu na uwezo walionao kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Hata hivyo, Dkt. Msafiri ameonesha kusikitishwa na hali ya baadhi ya vijana wa sasa kutokuwa na ari ya kujishughulisha na masuala ya maendeleo ya jamii. Dkt.Msafiri ameeleza kuwa vijana wana nafasi kubwa ya kufanya ubunifu na kuanzisha miradi itakayoboresha maisha yao na ya jamii kwani akili zao bado zinauwezo mkubwa.

Naye Ndg. Stanley Jeremiah kutoka Shirika la Uhifadhi wa Mazingira la SECO, ametoa mafunzo kuhusu namna vijana wanavyoweza kutambua fursa za kiuchumi zinazotokana na utunzaji wa mazingira, pamoja na kutumia majukwaa mbalimbali yaliyoandaliwa na Serikali na vikundi vya kukopeshana kupata mitaji ya kuanzisha shughuli za kiuchumi. Amesema zipo fursa nyingi za kiuchumi zinazoweza kupatikana kupitia shughuli za uhifadhi wa mazingira, akitolea mfano ukusanyaji wa makopo ya plastiki na kuyauza kwa wanunuzi wakubwa, hatua inayoweza kuwa chanzo cha kipato kwa vijana huku ikichangia utunzaji wa mazingira.

Kwa ujumla, mafunzo hayo yamelenga kuwajengea vijana kutoka dini mbalimbali uelewa kuhusu umuhimu wa upendo, haki na amani, pamoja na kuwahamasisha kutumia fursa zilizopo katika jamii zao kwa ajili ya maendeleo yao na jamii kwa ujumla.