PROF. DKT. JANET LEFROID AZURU DAYOSISI YA KASKAZINI BAADA YA TAKRIBANI MIAKA 36 UTUMISHI 

Leo Oktoba 22, 2026, Profesa Dkt. Janet Lefroid ametembelea Ofisi Kuu ya Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), alikohudumu kwa takribani miaka 11 katika Kitengo cha Elimu ya Afya ya Msingi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Prof. Lefroid alieleza furaha yake kurejea katika eneo ambalo alilitumikia kwa miaka mingi, akibainisha kuwa kipindi cha utumishi wake kilikuwa na changamoto mbalimbali za kiafya zilizohitaji juhudi kubwa katika kuelimisha jamii.
Alikumbuka kuwa mwaka 1989, jamii ilikabiliwa na changamoto kubwa iliyotokana na kuenea kwa ugonjwa wa UKIMWI. Kwa mujibu wa maelezo yake, yeye na wenzake walitumia muda mwingi kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kuwahudumia watu wanaoishi na VVU na wagonjwa wa UKIMWI.
Aidha, alieleza kuwa kazi yao ilihusisha utoaji wa elimu kuhusu afya ya uzazi, uzazi wa mpango na magonjwa ya kuambukiza. Vilevile, walijihusisha na kufundisha masomo ya afya ya kiroho, hatua iliyolenga kuimarisha ustawi wa jamii kwa kuzingatia afya ya mwili na roho.
Prof. Lefroid alieleza kufurahishwa kwake kuona kuwa baadhi ya kazi na mipango waliyoianzisha inaendelea kutekelezwa hadi sasa.
“Ninafurahi sana kuona kwamba baada ya kuondoka kwa miaka mingi ninakuta kazi tulizozifanya zikiendelea vizuri. Hili linanipa furaha kubwa,” alisema Prof. Lefroid.
Akimpokea Prof. Lefroid, Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Dkt. Fredrick Shoo, alieleza kufurahishwa kwake na mchango mkubwa alioutoa katika kipindi cha utumishi wake ndani ya Dayosisi.
Askofu Shoo alikumbuka changamoto zilizokuwepo wakati wa kutoa elimu kuhusu uzazi wa mpango, akibainisha kuwa suala hilo lilionekana kuwa mwiko katika baadhi ya maeneo ya jamii. Hata hivyo, alisema juhudi za kutoa elimu na kuhamasisha jamii zilisaidia kuleta mafanikio katika kampeni hiyo.
Katika nafasi hiyo, Askofu Shoo alitoa wito kwa jamii kuzingatia uzazi wa mpango kwa lengo la kuhakikisha wazazi wanapata nafasi ya kulea na kuwahudumia watoto wao ipasavyo.
“Ni jambo jema kuzingatia uzazi wa mpango na kuzaa watoto ambao utaweza kuwahudumia,” alisema Askofu Shoo.
Baada ya utumishi wake katika Kitengo cha Elimu ya Afya ya Msingi cha Dayosisi ya Kaskazini, Prof. Lefroid aliendelea na shughuli za kitaaluma nchini Uingereza, ambako alifundisha katika Chuo Kikuu cha Keele, akijikita katika masomo ya afya ya jamii na uongozi, pamoja na kushiriki katika tafiti mbalimbali.
Kwa sasa, Kitengo cha Elimu ya Afya ya Msingi cha Dayosisi ya Kaskazini kinaongozwa na Bibi Isaria Megiroo, ambaye anaendeleza majukumu ya kitengo hicho katika kutoa elimu ya afya na kuhamasisha ustawi wa jamii.
Ziara ya Prof. Dkt. Janet Lefroid ni fursa ya kutambua mchango wa watumishi waliolitumikia Kanisa na jamii kwa muda mrefu, pamoja na kuthamini mwendelezo wa kazi za elimu ya afya na huduma kwa jamii ndani ya Dayosisi.