ASKOFU SHOO AZINDUA JENGO LA IBADA LA BILIONI 6.5, MALASUSA ATOA WITO WA MALEZI NA UPATANISHI

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Dkt. Fredrick Onael Shoo, amezindua rasmi jengo jipya la kisasa la Ibada la Bethel, Usharika wa Nshara, lililogharimu takribani shilingi bilioni 6.5, huku Mkuu wa KKKT, Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa, akiongoza ibada ya uzinduzi na kutoa wito wa kuimarishwa kwa malezi, maadili mema na upatanishi katika familia na jamii.

Uzinduzi huo umefanyika Novemba 1, 2026, ukihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, viongozi mbalimbali wa Serikali, wa dini na waumini. Akihubiri katika ibada hiyo, Askofu Malasusa amewataka Wakristo kuishi maisha matakatifu, kuwa wanyenyekevu, kutambua makosa, kutubu, kuwa na kiu ya Neno la Mungu na kujiepusha
na majivuno huku wakiendeleza kuyaishi mafundisho ya Yesu Kristo.  Aidha, amewataka waumini kuwa wapatanishi badala ya wagombanishi, akieleza kuwa huduma hiyo inapaswa kuanzia katika familia, kwaya, mabaraza ya wazee na maeneo mengine ya
kijamii.

Akizungumzia jengo hilo, Askofu Malasusa ameipongeza Dayosisi ya Kaskazini kwa usimamizi wa ujenzi na kueleza kuwa ubora wake unaonesha thamani ya fedha zilizotumika. Pia amefurahishwa na ushiriki wa watu wa madhehebu na dini mbalimbali, wakiwemo Waislamu, katika kuchangia ujenzi huo, akisema ni ishara ya mshikamano katika jamii.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Mhe. Mwigulu Nchemba amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini, akitambua mchango wake katika utoaji wa huduma za elimu, afya na maendeleo ya kijamii. Amesema Rais amemtuma kuwasilisha salamu zake kwa viongozi wa Kanisa na kuwa hakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini, ikiwemo kushughulikia changamoto za kisera, kikodi na madeni, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika huduma za elimu na afya. Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameongoza harambee iliyohusisha Ofisi ya Waziri Mkuu na marafiki zake, iliyofanikiwa kuchangisha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuendeleza Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCo). Pia amesisitiza hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuhimiza upandaji miti, huku akieleza kuwa hoja zilizowasilishwa zitapokelewa na kufanyiwa kazi.

Ujenzi wa kanisa jengo hilo ulianza mwaka 2016 na kugharimu takribani shilingi bilioni 6.5, fedha zilizotokana na michango ya waumini, marafiki wa ndani na nje ya nchi pamoja na watu wa madhehebu na dini mbalimbali. Jengo hilo lina uwezo wa kuchukua waumini wapatao 2,000 na lina vyumba vya Shule ya Jumapili, mazoezi ya kwaya, ofisi za idara mbalimbali na kumbi za mikutano.