Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Dkt. Fredrick Onaeli Shoo, amefungua rasmi Kikao Kazi cha mwaka cha utendaji cha Wachungaji wote wa Dayosisi hiyo kinachofanyika katika Hoteli ya Uhuru Lutheran Hotel, leo Novemba 25, 2026.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho, Askofu Shoo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma ya Udiakoni, akiwahimiza wachungaji kuendelea kutambua na kuwahudumia watu wenye mahitaji mbalimbali katika jamii kama sehemu muhimu ya utume wa Kanisa.
Amesema kuwa mahitaji katika jamii ni makubwa, ingawa wakati mwingine yanaweza yasionekane kwa urahisi. Akitolea mfano wa kuanzishwa kwa huduma ya Building a Caring Community (BCC) inayolenga kuwahudumia watoto wenye ulemavu wa akili, amesema kuwa mwanzoni watu wengi hawakutambua ukubwa wa uhitaji uliokuwepo, lakini baada ya huduma hiyo kuanza, uhitaji huo umeonekana kuwa mkubwa zaidi.
Aidha, Askofu Shoo amewahimiza wachungaji na waumini kwa ujumla kutokudharau mchango mdogo katika kuwasaidia wenye mahitaji, akisisitiza kuwa si lazima msaada uwe mkubwa ili uwe na maana. Amesema hata kile kidogo kinachotolewa kwa moyo wa upendo kinaweza kuwa na maana kubwa na kuleta mabadiliko katika maisha ya watu wanaohitaji msaada.
Ameeleza kuwa Kanisa lina wajibu wa kuonesha upendo wa Kristo kwa vitendo kupitia huduma za huruma, mshikamano na kuwajali watu walio katika mazingira magumu.
Akihitimisha hotuba yake, Askofu Shoo amewataka wachungaji kushiriki kikamilifu katika mada zitakazowasilishwa wakati wa kikao kazi hicho pamoja na mijadala ya vikundi, ili kuhakikisha wanapata maarifa na uzoefu utakaosaidia kuimarisha huduma ya Kanisa.
Kikao kazi hicho ni sehemu ya juhudi za Dayosisi ya Kaskazini katika kuimarisha huduma ya kichungaji na udiakoni kwa ajili ya kulijenga Kanisa lenye upendo, mshikamano na linalowajali watu wote katika jamii.

