Askofu Dkt. F. Shoo Achaguliwa tena Miaka Sita

Mkutano mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini uliofanyika tarehe 30.08.2024, umemwomba Askofu Dkt. Fredrick Shoo, kuendelea na nafasi ya Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini kwa miaka mingine sita.

Mkutano huo pia umemchagua tena Msaidizi wa Askofu Mch. Msanya kwa kura na kupita kwa zaidi ya asilimia 97, kuendelea na nafasi yake kwa miaka mingine minne.

Mkutano mkuu hufanyika kila baada ya miaka miwili hivyo utafanyika tena mwaka 2026. Mkutano huu huhudhuriwa na wawakishi kutoka katika makundi mbalimbali katika sharika zote za Dayosisi. KKKT Dayosisi ya Kaskazini ina sharika 173, kila usharika hutuma wawakilishi wawili au zaidi kulingana na ukubwa wa usharika.

Huwepo pia na wawakilishi kutoka katika vituo vyote vya Dayosisi, Maaskofu kutoka Dayosisi za jirani, wageni kutoka serikalini mfano, Mkuu wa Mkoa ama Mkuu wa Wilaya pamoja na wawakilishi kutoka katika madhehebu mengine rafiki wa Dayosisi ya Kaskazini.

Mkutano Mkuu ni chombo cha juu kabisa cha maamuzi katika uongozi, ndicho kinachosimamia uongozi wa Dayosisi ya Kaskazini.

Katika kikao hicho, watendaji wa Dayosisi wanawajibika kueleza Mkutano mkuu kuhusu maendeleo, changamoto na utekelezaji wa maazimio ya mkutano uliopita.

Mkutano Mkuu pia unahusika katika uchaguzi wa viongozi wa juu, Halmashauri Kuu na Halmashauri zingine.