BAADA YA MIAKA 40 YA UTUMISHI, MCHUNGAJI SARA URASSA ASTAAFU RASMI.

Mchungaji Sara Urassa, mmoja wa wanawake sita wa kwanza kubarikiwa kuwa wachungaji KKKT Dayosisi ya Kaskazini, amestaafu rasmi  baada ya maiaka 40 ya utumishi na miaka 35  ya uchungaji.

Ibada ya maalumu ya kustaafishwa kwake imefanyika siku ya tarehe 20 Septemba, 2026 katika Usharika wa UUWO ikiongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dkt. Frederick Shoo.

Neno katika ibada hiyo lilisomwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira, Mch. Dkt. Angela Olotu, ambae amefundisha kuhusu huruma ya Mungu na kuongeza kuwa kustaafu kwa Mch.Sara ni huruma za Mungu tu.

Dkt.Olotu aliongeza kuwa kustaafu si mwisho wa huduma, bali ni mwanzo wa hatua nyingine ya kuendelea kumtumikia Mungu.

Katika ibada hiyo, Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Mhandisi Zebadia Moshi, alisoma historia ya Mchungaji Sara Urassa, ikieleza safari yake katika huduma ya Kanisa na nafasi yake miongoni mwa wanawake sita wa kwanza kubarikiwa kuwa wachungaji.

“Sara Urassa alibarikiwa kuwa mchungaji tarehe 4 Agosti, 1991 katika Usharika wa Moshi mjini, Mch. Sara alivyobarikiwa kuwa mchungaji, hili lilikuwa kundi la kwanza la Watheolojia sita wanawake kubarikiwa kuwa wachungaji katika Dayosisi yetu na Kanisa letu” alisema Mhandisi Moshi.

Akizungumza katika ibada hiyo, Askofu Frederick Shoo amesisitiza umuhimu wa wanawake kuendeleza huduma ya kichungaji, akieleza kuwa nafasi hiyo ina umuhimu katika kazi ya Kanisa.

Aidha, Askofu Shoo amemtaka Mchungaji Sara Urassa kuendelea kuwa sehemu ya kuwashauri na kuwaombea wanawake wanaohudumu kama wachungaji, hata baada ya kustaafu rasmi.

“Popote ulipopita uliacha alama ya utumishi wako, na sasa tunakuombea baraka za Mungu katika kustaafu kwako, sasa uendelee kuwashauri, kuwaombea wachungaji vijana ili huduma hii isiharibike, na huko ndiko kustaafu kwema na kuzeeka kwa amani” alisema Askofu Dkt.Shoo.

Kwa upande wake Mchungaji Sara baada ya kustaafishwa rasmi, amesoma itikio la kustaafu, akieleza shukrani zake kwa Mungu, Kanisa na wote walioshiriki katika safari yake ya huduma.

“Ninawashukuru sana Usharika huu, Mchungaji Kiongozi asante, washarika wote na kila mmoja aliefika kwa zawadi mlizonipa. Mimi namshangaa Mungu sana, na ndivyo Mungu anavyotenda, na kwa unyenyekevu naomba Mungu aendelee kuwabariki. Mungu wa Mbinguni asiwapungukie, asante sana kwa kunihesabu wa thamani”

Tukio la kustaafu kwa Mch.Sarah limehudhuriwa na watu kutoka makundi mbalimbali, washarika wa Uuwo, na kutoka sharika nyingine za Dayosisi ya Kaskazini, Wachungaji, kwaya mbalimbali na viongozi wa serikali.