BCC WAADHIMISHA KILELE CHA MWEZI WA AFYA KWA KUPIMA AFYA NA IBADA YA REJOYCE SPIRIT

Kitengo cha Building a Caring Community, BCC kilichopo chini ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini kimeadhimisha siku ya kilele cha mwezi afya kwa kuwafanyia vipimo Watoto wenye ulemavu wa viungo na kwa ibada maalumu.

Tukio hilo limefanyika tarehe 29 septemba 2026, KKKT Usharika wa Rau,uliopo Moshi, Kilimanjaro, ambapo Watoto wanaolelewa na vituo mbalimbali vya BCC wame fanyiwa vipimo vya kitabibu ili kujua maendeleo yao.

Mgeni rasmi wa tukio hilo ambae ni msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya kaskazini, Mch.Deogratius Msanya ametoa pongezi kwa wazazi kwa kuchukua uamuzi mzuri wa kuwaleta Watoto wao kupata msaada katika vituo vya BCC

Mch.Msanya ametoa wito kwa watoa huduma, kuwahudumia kwa upendo Watoto wenye ulemavu, kwani kazi hiyo ni huduma yenye baraka na inayohitaji kutozimia moyo.

Naye Sabina Manoi ambae ni mmoja wa wazazi wa watoto walionufaika na huduma za BCC ameishukuru BCC kwa kuwahudumia Watoto wenye ulemavu hasa kwenye masuala ya kiafya, kwani Watoto wengi wamekatiwa  bima za afya.

Katika tukio hilo, serikali imewakilishwa na Dunkan Mgati, Afisa mkuu wa ustawi wa jamii kutoka manispaa ya Moshi, ambae ameeleza historia ndefu na mchango wa BCC katika ustawi wa jamii, huku akieleza namna taasisi hiyo imekua msaada kwa wanawake wenye Watoto wenye ulemavu mbalimbali sambamba na upimaji wa toto BCC wametoa huduma ya vipimo mbali mbali vya afya kwa wazazi na wageni waliofika katika tukio hilo.

Katika Ibada ya Rejoyce Spirit Mchungaji Kileo ametoa Neno huku akisema Yesu Kristo anafundisha kwamba watoto ni wa thamani mbele za Mungu, licha ya kuwa na changamoto mbalimbali, huku akiwatia moyo wazazi kwamba watoto wao ni wa thamani.

Mratibu wa BCC, Mdiakonia Elirehema Kaaya, amesema huduma hiyo inalenga kuhamasisha ujumuishi na kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kuwajumuisha vijana wenye mahitaji maalumu katika jamii. Kwa upande wake, mzazi mmoja kwa niaba ya wazazi wengine ametoa shukrani kwa BCC kwa kuwahudumia watoto wao katika nyanja mbalimbali.