Taasisi ya Bishop Martin Fuatael Shao (BMFSF) inayotoa misaada ya elimu, matibabu, mavazi, na chakula hususani kwa watoto, imesaidia zaidi ya familia 4000 katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kilimanjaro na Karatu mkoani Arusha.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa vyakula, nguo na taulo za kike kwa familia zinazoishi katika mazingira magumu, lililofanyika kuanzia Juni 06 hadi mwanzoni mwa mwezi Julai 2021, katibu wa taasisi hiyo Bw.Ebenezer Shao alisema taasisi hiyo pamoja na huduma za upimaji afya za watoto na matibabu pia wanawakatia watoto Bima za afya kuwasaidia kupata matibabu kwa urahisi.
Kwa nyakati tofauti mwezi Juni hadi Julai mwazoni katika maeneo ya Lemira Kati, Masama, Lukani, Ng’uni {wilaya ya Hai}, Lole na Kyomu {wilaya ya Moshi vijijini,} familia zaidi ya 80 zimepokea misaada ya chakula, mavazi na taulo za kike
“Katika mwezi Juni na Julai mwanzoni kupitia bodi yetu tumeandaa na kugawa vyakula, mavazi na taulo za kike kwa familia zaidi ya 80 na lengo letu ni kufikia familia nyingi zaidi zenye uhitaji” Alisema Ebenezer.
Amesema kwa kila familia wamegawa mchele kilo 5, unga wa dona kilo 5, sabuni, mafuta ya kupika, nguo, viatu pamoja na taulo za kike.
Hata hivyo ameeleza kuwa, taasisi hiyo imelenga kutoa misaada kwa jamii hususani watoto katika elimu, matibabu,chakula na makazi wakishirikiana na kamati za matendo ya huruma(Udiakonia) zilipo katika Sharika za Dayosisi.
Mbali na matibabu amesema kwa sasa taasisi hiyo tayari imekwisha saidia ada na sare za shule kwa watoto zaidi ya 30 wa shule za msingi, 25 wa Sekondari, 2 wa vyuo vya Kati, 6 wa vyuo vya ufundi na 2 wa chuo kikuu.
Muasisi wa taasisi hiyo Askofu Dkt. Martin Fuatael Shao wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini (Mstaafu) akizungumza na baadhi ya familia hizo alisema wanapaswa kuishi kwa matumaini wakitambua kuwa Mungu anawapenda na ndiyo sababu Kanisa na watu mbalimbali wanajihusisha na maisha yao.
“Tumefika kuwasalimu na kuwaletea ujumbe kuwa Mungu anawapenda, mnapopita katika changamoto nyingi msidhani kuwa Mungu amewasahau, Mungu anawapenda siku zote na ndiyo sababu ametutuma kudhihirisha upendo wake kwenu alisema.” Askofu Shao.
Alihimiza binadamu kupendana na kusaidiana kama njia pekee ya kumtumikia Mungu na kudhihirisha upendo wa Mungu kwa wanadamu wote.
Aidha alimshukuru Mungu kwa upendo wake uliowawezesha kuanzisha taasisi hiyo kwa ajili ya kuwahudumia watu wanaoishi katika mazingira magumu na kutoa wito kwa jamii kupendana na kusaidiana.
Baadhi ya familia zinazopita katika changamoto za kimasha walizungumza na gazeti la Upendo; Bibi Advesar Anderson Mringo (92) mjane wa mzee Anderson Mringo hawezi kutembea amelala kitandani kwa muda mrefu, aliishi kwa kumtegemea mtoto wake Namweli Mringo wakati ana nguvu za kufanya kazi.
Namweli alijishughulisha na ufundi cherehani na aliweza kumtunza mama yake na familia yake pia lakini, mwaka jana (2020) aliugua na kupooza hali iliyosababisha familia hiyo kuishi katika mazingira magumu. zaidi baada ya kulala kwa muda mrefu amepata maradhi ya sukari na presha.
Hali hii imeifanya familia kuishi katika hali ngumu akimtegemea mkewe kuitunza familia kwa tabu kwa kufanya vibarua na misaada midogo midogo kwa jamaa. Matibabu yamekuwa ni changamoto.
Bw. Namweli anaishukuru taasisi ya Askofu Shao kwa msaada na kuahidi kufuatilia afya yake kwa kushirikiana na Usharika wa Lole. Anatoa wito kwa jamii kuendeleza roho ya upendo na kusaidi familia zinazopita kati hali ngumu ya maisha.
Bibi Lightness anaishi na wajukuu 4, mume wake na watoto wake wamefariki, anakaa na wajukuu wake 4 wanaomtegemea. Anasema hali ya Maisha ni ngumu, wanategemea kupata chakula kwa kuponda kokoto na kuuza. Anashukuru taassisi ya Askofu Shao kwa msaada. “Namshukuru Askofu kwa msaada aliotupa, hali ni ngumu, chakula shida, wajukuu wanahitaji kwenda shule, namwombea aendelee kutusaidia sisi wanyonge”Alisema Bibi Lightness.
Naye Mwenyekiti wa Udiakonia Usharika wa Lole wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Jimbo la Kilimanjaro Mashariki Bw. Ndengirio Mringo anasema uhitaji wa watu wanaoishi katika mazingira Magumu ni Mkubwa.
Anasema wao kama kamati ya Udiakonia katika Usharika wametoa misaada ya matibabu, bima ya afya, ada, chakula, mitaji ya mbuzi wa maziwa kwa kaya Zaidi ya 80 kwa mwaka huu wa 2021.
