IDARA YA MAWASILIANO KKKT DK YAFANYA SEMINA UTUNZAJI WA KUMBUKUMBU ZA KANISA

Idara ya Mawasiliano KKKT Dayosisi ya Kaskazini imeendesha semina maalumu ya kutambua umuhimu na namna ya kutunza kumbukumbu za Kanisa.

Semina hiyo imefanyika tarehe 25 Septemba,2026  katika ukumbi uliopo Lutheran Uhuru Hotel ikihudhuriwa na wajumbe kutoka sharika za Dayosisi hiyo.

Mchungaji Enock Makundi ambae ni Mratibu kutoka kitengo cha kutunza nyaraka za kumbukumbu, Makavazi kilichopo makao makuu ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini, ametoa elimu kwa wajumbe kuhusu namna ya kutunza kumbukumbu, na ni kumbukumbu gani zinafaa kutunzwa.

Mchungaji Makundi ameeleza kuwa umuhimu wa kutunza kumbukumbu za Kanisa hauishii kwenye karatasi tu, bali hata majengo na vitu ambavyo vina historia fulani katika Kanisa.

Utunzaji wa kumbukumbu za kanisa unaweza pia kuwa sehemu ya kuingiza kipato katika sharika na Dayosisi kwani kwa wengine ni sehemu ya utalii, hivyo mtu anaweza lipia ili kuja kuona na kujifunza mambo mbalimbali ya kihistoria kuhusu kanisa, aliongeza Mch.Makundi

Baadhi ya wajumbe walioshiriki semina hiyo, wameonesha kufurahishwa na elimu waliyoipata kuhusu utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu za Kanisa.

“Kwakweli siku ya leo nimefurahishwa sana na nilichokikuta, imekua kama utalii na chachu ya kwenda kuwaambia wengine namna ya kwenda kutunza kumbukumbu katika namna itasaidia vizazi vitakavyokuja” amesema Marry Malisa mmoja ya wajumbe wa semina hiyo.

Naye Mhandishi Ekaeli Manase ambae pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya mawasiliano ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini na mjumbe wa semina iliyofanyika, amepongeza kufanyika kwa semina hiyo, huku akitoa wito kwa sharika kutunza kumbukumbu hizo na kutambua umuhimu wake kabla hazijapotea.

“Natamani kila aliehudhuria semina hii aende kusimama katika Sharika na Jimbo lake alikotoka kuleta mabadiliko, ili taarifa zote zilizomuhimu zitunzwe, historia isipotee. Pasipo kutunza kumbukumbu historia inapotea, lakini kila mtu akitunza kumbukumbu vizuri, tutaweka historia ya kanisa letu vizuri” alisema Mhandisi Manase

Akihitimisha semina hiyo, Mch. Makundi ametoa shukurani kwa uongozi wa Dayosisi ya Kaskazini na wajumbe wa semina hiyo kwa kufanikisha kufanyika kwa semina hiyo.