Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, amewataka Wainjilisti kutumia nafasi yao kuhamasisha jamii kupata watu wema, waadilifu na bora watakaoingia katika kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.
Akofu shoo aliyasema hayo Jimboni Karatu wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wa Kiuchumi, Miradi na Ufahamu kuhusu vipaumbele vya Mpango Mkakati wa Dayosisi kwa Wainjilisti wote wa Jimbo la Karatu iliyofanyika Juni 5, 2024 Jimboni Karatu.
Pia alisema wanapaswa kuhamasisha watu kuhakiki majina yao katika zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura na kuhakikisha majina yao yapo.
Aidha aliwakumbusha Kutambua na kutunza heshima ya huduma walioitiwa kwani huduma yao inaumuhimu mkubwa katika kumzalia Mungu matunda mema.
“Niwaombe mtumie fursa ya huduma hii kuleta mabadiliko ya kiroho na kimwili hasa Uchumi katika kilimo na ufugaji na kuzingatia kuwa suala la Utunzaji wa mazingira ni jambo la kila mmoja. Tutunze mazingira kwa kuotesha miti ya asili na ya matunda katika kaya, mitaa na Sharika zetu”.Alisema Dkt. Shoo