Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kupitia Kurugenzi ya Afya na Diakonia, imeendesha semina ya siku mbili ya mapitio na uzinduzi wa kitabu ambacho ni kitendea kazi cha kufundishia afya ya uzazi, jinsia na haki kwa vijana.
Semina hiyo iliyohusisha Dayosisi tatu za KKKT ambazo ni Dayosisi ya Kaskazini, Dayosisi ya Kaskazini Kati na Dayosisi ya Meru, imemalizika leo Oktoba 13, 2026 mjini Moshi Kilimanjaro katika ukumbi wa Lutheran Uhuru Hotel huku ikijumuisha wajumbe na Maaskofu kutoka Dayosisi hizo.
Akizungumza alipopewa nafasi ya kuzindua kitabu hicho, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dkt.Fredrick Shoo amesema Dayosisi hizo zimekipokea kitendea kazi hicho kama nyenzo muhimu ya kufundishia.
“Tumesikia yaliyomo ndani yake, na tumekikubali kabisa kitabu hiki” aliongeza Askofu Shoo.
Askofu Shoo ameeleza kuwa kitendea kazi hiki kitasaidia katika kutoa elimu ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana.
Aidha, Dkt. Zebadia Mbando, Mkurugenzi Huduma za Afya na Diakonia KKKT amesema kitendea kazi hiki kitasaidia vijana kufundishwa juu ya kutawala afya zao,jinsia, afya ya uzazi na haki, na namna ya kuishi zama zenye magonjwa mengi kama UKIMWI, magonjwa ya akili na madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya.
Sambamba na hilo, Mwl.Magdalena John, Katibu idara ya Wanawake na Watoto KKKT, ametoa shukurani kwa kupata mafunzo hayo, huku akiahidi kua balozi mzuri wa kufundisha vijana katika Dayosisi anayotoka.
Akihitimisha semina hiyo, Mwl. Solomon Loshilu Sambweti ambae ni Katibu Mkuu Dayosisi ya Kaskazini Kati na mwenyekiti wa mafunzo, amewasisitiza wajumbe kuitendea mipango yote iliyowekwa katika semina hiyo, na si kuiacha kwenye karatasi pekee.






