Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, ameongoza Ibada ya kumstaafisha kwa heshima Mkuu wa pili wa Jimbo la Hai Mch. Anasael Massawe, Ibada iliyofanyika katika Usharika wa Hai Mjini September 24, 2023.
Akitoa salam za Kanisa na Dayosisi Askofu Dkt. Shoo alimpongeza Mch. Anasael Massawe kwa utumishi wake hadi kufikia muda wa kustaafu kwa heshima pamoja na wote walioshiriki katika kufanikisha tendo hilo la kustaafu kwake.
Pia alitoa Salam kutoka Krakow-Poland alipohuzuria Mkutano Mkuu wa 13 wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (LWF) mwishoni mwa mwezi Septemba 2023.
Alisema miongoni mwa mambo yaliyokazwa katika Mkutano huo ni pamoja na Umoja. Anasema walikaza kuwa wote ni wamoja ndani ya Kristo na isitokee mifarakano katika Kanisa, katika familia za Kikristo wakitambua kuwa wote ni viungo katika mwili wa Kristo.
Pia walikaza juu ya Roho mmoja wakitambua kuwa zimetokea roho nyingi za mapepo. “Tulihimiza kuwa tunapaswa kutambua sisi tunamtambua Roho mmoja wa Kristo na tumwombe Kristo atuwezeshe kuweza kupambanua na kutambua hizi roho nyingine” Alieleza Askofu Dkt. Shoo
Jambo la tatu walikaza tumaini moja yaani mwili mmoja, Roho mmoja na tumaini moja ambapo walisema wanatambua kuwa sote ni Wakristo na wanapaswa kusimama katika tumaini moja katika maisha ya sasa na yale ya tumaini lijalo pamoja na mambo mengine kama utunzaji wa mazingira na kudumisha Amani.
Katika Mkutano huo pamoja na kuchaguliwa kwa raisi wa LWF Askofu Henrik Stubkjær
kutoka Kanisa la Kilutheri la Denmark pia Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya LWF.
Katika Ibada hiyo Mkuu wa Jimbo la Siha Mch. Elisa Kileo alihubiri ambapo somo lilitoka katika kitabu cha Luka 4:31-37.
Akihubiri na kutoa mfano wa Petro alivyopitia changamoto katika kumtumikia Mungu na kupelekea kufungwa na hatimaye malaika wa Mungu akamtoa gerezani; alisema safari ya maisha inachangamoto nyingi haswa kwa watu wanaomwamini na kumkiri Yesu kuwa ni Bwana na Mwokozi wa Maisha.
Alisema kuna vita vikali kati ya ufalme wa Mungu na ufalme wa Shetani ambapo falme hizo haziwezi kukaa pamoja. Duniani Kuna vita vingi kati ya watu wa Mungu na wafuasi wa shetani na hii inasababisha kuwepo kwa changamoto nyingi katika maisha hapa duniani.
Alimpongeza Mch. Masawe kwa kustaafu kwa heshima na kuusema kuwa ni jambo la kumshukuru Mungu pale mtumishi anapomaliza wito wa utumishi wake salama.
“Watumishi mtambue kuwa mnawindwa sana na mwovu ili awaondoe katika ile kazi Mungu aliyowaitia hivyo mvipige vita vizuri vya Imani na mjue mnalotumaini. Tumaini letu ni kukaa ndani ya neno la Mungu na kumwomba Mungu”. Alihitimisha Mch. Kileo
Mch. Massawe alianza huduma ya Uchungaji mwaka 1998 na alitumika katika sharika mbaklimbali hadi alipofikia muda wa kustaafu akiwa ni Mch. wa Usharika wa Fuka