Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mch. Deogratius Msanya, alifungua maadhimisho ya siku ya Wajane Duniani Kanda ya Kaskazini Juni 20, 2023. Maadhimisho hayo yaliandaliwa na Chama cha Wajane Tanzania kanda ya Kaskazini (TAWIA) wakishirikiana na Dayosisi ya Kaskazini.
Siku ya wajane duniani huazimishwa kila mwaka tarehe 23 Juni, ambapo kila kanda ina siku yake kabla ya kufanyika maadhimisho ya kitaifa. Kanda ya Kaskazini wameazimisha tarehe 20.06.2023 katika Manispaa ya Moshi Mjini Jimbo la K/Kati la KKKT Dayosisi ya Kaskazini.
Akiongoza sala ya asubuhi kabla ya kufunguliwa rasmi kwa maadhimisho hayo, Mkuu wa Jimbo la K/Kati Mch. Javason Mrema alisema safari ya maisha ya wajane ni ya kipekee na ni ngumu japo wanaye Yesu wanayemtegemea. Kuna kuwa na dhoruba nyingi katika safari ya wajane kama changamoto za ukoo, malezi, madeni n.k alieleza.
Alisema pamoja na changamoto na dhoruba mbalimbali katika maisha ya ujane wakimtegemea Yesu na kumruhusu aingie katika nyumba zao na maishani mwao; dhoruba na mizigo waliyonayo itatulia na kuisha kama Yesu alivyoingia chomboni wakati wa dhoruba kule baharini na chombo kikatulia.
“Mungu anaporuhusu mwenzi wako kukuacha, anajua namna atakavyokutunza na daima utashinda. Kamwe usiingiwe na hofu maana ukiogopa shetani atakuzamisha kama Petro alivyokuwa akitembea juu ya maji baharini na baada ya kuwa na hofu akaanza kuzama”.Alisema Mch. Mrema
Akisoma risala mbele ya Mgeni rasmi Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya; mratibu wa TAWIA Kanda ya Kaskazini Bibi. Mercy Ndosi aliwaambia wajane wasikate tamaa katika maisha maana Mungu siku zote anashughulika na maisha yao na kamwe hawezi kuwaacha pale wanapomtegemea.
Alisema chama cha TAWIA kina miaka 8 hadi sasa na kuwataka wajane kuwa na umoja, mshikamano na kuendelea kuwa wanachama wa chama hicho. Awali alilishukuru Kanisa kwa kufanya kazi nzuri ya udiakonia katika kuwahudumia wajane.
Bibi Mercy alisema Maadhimisho hayo ni ya nane kwa hapa Tanzania na ni ya 25 kimataifa. Alisema wameweka utaratibu wa wajane wote nchini kukutana kila baada ya miaka mitano kwaajili ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusiana na haki, maslahi yao, kuunda umoja wao na kufahamiana kwa kuwaleta karibu.
“Siku hii imekuwa jukwaa la sauti za wajane. Tunamshukuru Mungu kwani mambo mengi yameweza kufanyika ikiwemo wajane kutambulika kama kundi maalum, mabadiliko ya sheria za mirathi, sera za wajane kupatikana kwa majukwaa ya wajane kuanzia ngazi ya kanda, mkoa, wilaya na kata”.Alisema Mercy
Akihitimisha hotuba yake Bibi Mercy alitoa ombi kwa Kanisa na kwa wadau mbalimbali kuendelea kuwapa ushirikiano ili kuendelea kuadhimisha siku hiyo kila mwaka na kuweze kuibua changamoto mbalimbali zinazowakabili wajane ili jamii ipate elimu na uelewa sahihi wa namna bora ya kuheshimu utu, haki na heshima ya makundi maalumu ya wajane, wagane, yatima n.k
Akitoa ushuhuda wa miaka 30 ya maisha ya ujane; Mch Verolise Mtei anasema anamshukuru Mungu kwa jinsi alivyompigania katika Maisha tangu aondokewe na mume wake.
Alisema wanapokutana wajane wanatiana nguvu hasa pale tunapoonana tukiwa wenye wafya njema, na hali nzuri ya maisha. Alieleza kuwa wakiwa na Yesu wanafaraja, nguvu na wanayaweza yote katika yeye awatiae nguvu.