TAMASHA LA MKUU WA JIMBO NA VIJANA 2026 SIHA LAFANA, KIJANA APEWA WAJIBU MZITO

Mkuu wa Jimbo la Siha, Mch. Elisa Kileo, amefungua Tamasha la Mkuu wa Jimbo na Vijana kwa kutoa wito kwa vijana kuwasaidia wenzao ambao wamepotea katika maadili kurudi kwenye mstari.

Tamasha hilo, linalofanyika mara moja kila mwaka, limezinduliwa tarehe 3 Oktoba 2026, katika Kanisa la KKKT Usharika wa Sanya Juu, Jimbo la Siha.

Akizungumza katika hotuba yake ya ufunguzi, Mch. Kileo ameeleza kuwa kuna ongezeko kubwa la vijana wasiokuwa na maadili, huku moja ya dalili kubwa ikiwa ni kutokujihusisha kwao na masuala ya ibada.

Mch. Kileo amesema vijana wengi wameyapa kisogo masuala ya ibada na badala yake wamegeukia mambo yasiyo na maadili, ikiwemo ulevi uliopindukia.

“Matendo haya yanaharibu nguvu kazi ya jamii kwani wengine wanafariki kabla ya wakati wao,” anasema Mch. Kileo.

Ameongeza kuwa kila kijana ana wajibu wa kutafakari namna ya kuwasaidia vijana wengine wanaopitia hali hiyo ili waweze kurudi katika mstari.

“Ni lazima kama kijana utafakari namna ya kuwasaidia vijana wengine warudi katika mstari,” ameongeza Mch. Kileo.

Tamasha la Mkuu wa Jimbo na Vijana linawakutanisha vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo la Siha, huku ujumbe mkuu ukiegemea katika kumshauri kijana kutambua hatima yake na kuchukua hatua zinazomsaidia kufikia maisha yenye mwelekeo mzuri.