“Tufanye Kazi ya Mungu Tukisukumwa na Upendo” Aliyasema hayo Bibi. Merry Mfuru Parish Worker wa Usharika wa Karanga kwenye maonyesho ya kazi za Idara ya Wanawake katika Usharika wa Shia mtaa wa Kameti.
Akizungumza na wanawake usharikani hapo Jumamosi Mei 28, 2021 alisema, wanawake wanapaswa kutambua kuwa kuwapo kwao katika idara na kupata fursa ya kumtumikia Mungu ni zawadi ya pekee kutoka kwa Mungu.
Amesema wafanye kazi hiyo kwa Moyo na kwa upendo wakitambua wanafanya kazi hiyo nyumbani mwa Mungu na ni heshima Mungu amewapa kumtumikia katika nyumba yake. “Fanya kazi ya Mungu kwa Upendo na Uaminifu bila kukata tamaa, usione haya au kudhani unafanya kazi ya Mungu kwa hasara, kutumika katika kanisa la Mungu si hasara hata kidogo.” Alisema Bibi.Mfuru
Aliwatahadharisha Wanawake Usharikani hapo kujihadhari na watu ambao wanabeza na kuwakatisha tama wanawake ambao wanajitoa katika kazi za Idara ya Wanawake.
Naye Mama Mwenyekiti wa Idara Usharika wa Bonite Bibi. Merry Muro aliwataka wanawake kutamani kutumika katika Kanisa la Mungu kwani ni heshima kwa Mungu. Alisema hata maandiko matakatifu yanasema kumtumikia Mungu kuna faida na ni heshima akinukuu neno kutoka kitabu cha Yohana 12:26 Mtu akinitumikia, na anifuate, nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo.Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.
Aidha katika Maonesho hayo, mbali na kazi za ubunifu, utunzaji mazingira, chakula bora, wanawake walijifunza wajibu wa mwanamke na mwanume katika kuijenga familia bora na malezi ya kuwaimarisha vijana na watoto.
