Uimbaji wa ngazi ya Jimbo umefanyika Oktoba 4, 2026, katika Jimbo la Kilimanjaro Kati, KKKT Dayosisi ya Kaskazini, ambapo kwaya 29 kutoka Sharika mbalimbali za Jimbo zimeshiriki.
Uimbaji huo umefanyika katika Usharika wa Lowiri na kuhudhuriwa na waimbaji pamoja na waumini kutoka katika Sharika mbalimbali za Jimbo hilo.
Akifungua rasmi uimbaji huo kwa niaba ya Mkuu wa Jimbo, Mchungaji Javason Mrema, ambaye yuko safarini, Mkuu wa Pili wa Jimbo, Mchungaji Israeli Moshi, amesema ameona utukufu wa Mungu kupitia uimbaji uliofanyika huku akizipongeza kwaya kwa ubunifu mkubwa walioonesha.
Mchungaji Moshi amesema anatamani ubunifu na bidii vilivyoonekana katika uimbaji huo viendelee kuonekana pia katika ibada za kawaida katika Sharika.
Amesema endapo waumini wataenda katika Sharika na kukuta kwaya zimejaa na zinaendelea kufanya vizuri katika ibada, itakuwa ishara kwamba wanachofanya katika mashindano haya si kwa ajili ya mashindano pekee, bali ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu.
Katika ibada hiyo, akihubiri, Mchungaji Fredrick Minja amesema Wakristo wanapaswa kumfuata Yesu Kristo na kuyafanya maisha yao kuwa sadaka kwa Mungu, kwa kuwa kwa Mungu yote yanawezekana.
Mchungaji Minja amesema thamani ya mwanadamu kuishi duniani ni kumfuata Yesu na kuishi maisha matakatifu. Amesema mtu akimfuata Yesu, atakuwa pamoja naye mahali alipo na ataheshimiwa na Mungu, hata kama dunia haitamheshimu.
Baada ya uimbaji huo, Mkufunzi Mstaafu wa Chuo Cha Mafunzo na Uongizi Usangi aliwataka walimu wa kwaya kuzingatia uwezo wa kwaya zao wakati wa kuchagua nyimbo za kushiriki katika uimbaji.
Aidha, katika kwaya zilizoshiriki katika makundi mbalimbali kama vile kwaya za watoto, vijana, wanaume, wanawake na mchanganyiko, zilitoka kwaya 7 zilizofuzu kwenda katika uimbaji ngazi ya Dayosisi.
Katika kundi la tarumbeta kwaya pekee katika kundi hilo ya Moshi Mjini ili fuzu, kwaya ya sekondari Mtakuja ilifuzu katika kundi la shule za Sekondari, watoto Washarika wa Emannuel Katanini walifuzu katika kundi la kwaya za watoto, katika kwaya za wanawake usharika wa Lowasi ilifuzu, kwaya ya wanaume Moshi mjini ilifuzu katika kundi la kwaya za wanaume, kwaya ya vijana Pasua ilifuzu katika kundi hilo na hatimae kwaya ya Usharika wa Rau ilifuzu katika kundi la kwaya mchanganyiko.
Kwaya hizi zinatarajiwa kukutana na kwaya kutoka majimbo mengine ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini ifikapo mwezi Oktoba 2026.






