Ofisi kuu ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Idara ya Afya Kitengo cha Afya ya Msingi, imeandaa semina ya siku tano ya kuwajengea uwezo waalimu 18 wa elimu ya afya ya msingi katika majimbo manne kuanzia tarehe 24-28.2.2025. Semina hiyo ilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Sun Marangu Retreat Center uliopo Marangu Moshi.
Walimu hao watahusika kuwajengea uwezo wenyeviti wa kamati za afya sharikani kwa lengo la kuelimisha washarika na jamii kwa ujumla ususan magonjwa yasiyoambukiza, wakishirikiana na wataalum wa afya waliopo katika maeneo yao. Watasaidia pia kuhamasisha upimaji wa afya ikiwemo magonjwa kama vile presha, kisukari, urefu na uzito na pia uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake na saratani ya tezi dume kwa wanaume.
Aidha, mambo walijifunza katika semina hiyo, ni masomo ya afya ikiwemo chanzo cha ugonjwa wa presha, kisukari; dalili za magonjwa hayo, namna ya kujikinga nayo. Walijifunza mbinu za kufundisha watu wazima kulingana na rika na utashi wao, kutumia mikutano ya hadhara na jumuiya kufikisha elimu hii, pia walijifunza mbinu za kutatua migogoro katika jamii na kufikia maridhiano.
Semina hiyo ya siku tano ilihitimishwa kwa wahitimu hao kuingizwa kazini na Mchungaji Exaud Makundi aliyemwakilisha Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya na kuwakabidhiwa vyeti vya kuhitimu tayari kwenda kuitumikia jamii. Walimu hao walianza kupata elimu hiyo ya afya ya msingi mwaka 2023 kwa siku tano na sasa wamekamilisha siku kumi za mafunzo na kuhitimu.

