Wasifu wa Hayati Askofu Dkt. Martin Fataeli Shao

KKKT Dayosisi ya Kaskazini imepata msiba wa kuondokewa na aliyekuwa Askofu wa Awamu ya Tatu Hayati Askofu Dkt. Martin Fataeli Shao.

Alizaliwa tarehe 18 Disemba, 1939 katika kijiji cha Lole, kata ya Mwika, wilaya ya Moshi- Vijijini. Mwaka 1966 – 1974 alikuwa Mchungaji wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini. Mwaka 1974 – 1976 alikuwa mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki. Mwaka 1976 – 2004 alikuwa Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini. Baadae alichaguliwa kuwa Askofu wa Awamu ya Tatu  KKKT Dayosisi ya Kaskazini ambako alihudumu kwa miaka 10 (2004 – 2014). Baada ya kustaafu alikabidhi uongozi kwa Askofu Dkt. Fredrick Shoo ambaye ndiye Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini hadi sasa.

Hayati Askofu Shao, alikuwa kiungo muhimu sana katika umoja wa kanisa, jumuiya za kanisa na taasisi za ndani na nje ya nchi. Katika uhai wake alianzisha kituo cha watoto wenye changamoto za afya ya moyo iliyoitwa Martin Fataeli Shao. Alitumikia kanisa na jamii kwa uaminifu, alijali sana mambo ya kiroho, alikuwa mtetezi wa haki na usawa. Tutamkumbuka kwa hekima, busara na moyo wa upendo aliouonesha wakati wote wa utumishi wake na hata baada ya kustaafu kwake.

Askofu Shao, alifariki dunia tarehe 25 Agosti 2025 akiwa na umri wa miaka 86.  Atazikwa tarehe 4 Septemba 2025.

Tutamkumbuka Daima