Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Dkt. Fredrick Onael Shoo, amegawa pikipiki 9 kwa Wachungaji toka sharika mbalimbali za Dayosisi kwa-ajili ya kurahisisha huduma sharikani.
Baba askofu amegawa pikipiki hizo kufuatia utaratibu uliowekwa na Dayosisi kupitia Idara ya Misioni na Uinjilisti ya kuwawezesha Wachungaji kupata pikipiki kwa njia ya uenyeji na kwa bei nafuu.
Pikipiki moja inagharimu kiasi cha shilingi milioni mbili na laki sita (2,600,000/=) na tayari ikiwa imekatiwa vibali vyote ambapo Mchungaji anapewa kwa unafuu wa nusu bei sawa na shilingi milioni moja na laki tatu (1,300,000/=) badala ya milioni mbili na laki sita.
Zoezi hilo limefanyika katika ofisi Kuu ya Dayosisi ya Kaskazini Julai 18, 2022 ambapo mchakato wake huratibiwa na ofisi ya Msaidizi wa Askofu ikishirikiana na ofisi ya Boharia.
Mhe. Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya akimkaribisha Baba Askofu kukabidhi pikipiki hizo alisema wamefanikiwa kununua pikipiki 9 ambazo atazikabidhi kwa watumishi hao.
Akigawa pikipiki hizo, Baba Askofu Dkt. Shoo alitoa wito kwa Watumishi hao kutumia vyombo hivyo kwa uangalifu na kwa ajili ya kufanikisha kazi ya Bwana. Anasema vyombo hivyo ni kwa ajili ya kuwasidia watumishi kuwafikia na kuwahudumia washarika kwa haraka na kwa mapana zaidi.
“Niwaombe Wachungaji mkavitumie vyombo hivi katika kufanikisha kazi ya Bwana na kuongeza ufanisi katika kazi” Alisema Askofu Dkt. Shoo.