MAHAFALI YA 25 AGAPE JUNIOR SEMINARY

Mahafali ya 25 ya kidato cha 6, ya shule ya Agape Junior Seminary ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini yamefanyika Mei 16, 2026 ambapo mgeni rasmi Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo alitoa vyeti kwa wahitimu. Awali aliongoza ibada ya kuweka jiwe la pembe jengo la Maktaba lenye madarasa ya Amali pamoja na ukumbi anuwai.

Akihubiri katika mahafali hayo, Askofu Dkt. Shoo, amesema kuwa kumekuwa na roho ya ukengeufu hasa kwa vijana, hadi kufikia hatua ya kutowasikiliza wazazi na viongozi wao. Amesema kizazi cha sasa kinaonekana kuamini kuwa kinajua kila kitu.

“Wazazi wako wamekulea katika imani thabiti, katika kumcha Mungu na katika mafundisho sahihi ya Bwana. Leo unaona mafundisho hayo ni ya kizamani sana. Muwe waangalifu, roho za udanganyifu zipo,” alisema Askofu Shoo.

Aidha, amesema kuna makundi yanayojulikana kama “Cult”, ambayo huwatoa watu katika imani waliyojengewa na kuwashawishi kumtii kiongozi mmoja anayewatenga na familia, wazazi pamoja na marafiki zao.

“Kundi hilo hukuexploit na kukufanya maskini kabisa. Mwisho wake baadhi ya watu hujikuta katika upweke, na wengine hata kuamua kujiua,” alisema.

Aliongeza kuwa viongozi wa makundi hayo hudai wamepata mafunuo, kisha kuyafanya mafunuo hayo kuwa amri za kuwaendesha waumini wao wanavyotaka.

Askofu Shoo amewataka wahitimu hao kuzingatia malezi na mafundisho waliyoyapata katika seminari hiyo, akisema yatasaidia kupambanua mitego ya shetani na kuishi katika msingi imara wa imani.