MAHAFALI YA 11 YA TAASISI YA MAFUNZO YA AFYA MACHAME

Taasisi ya Mafunzo ya Afya Machame imefanya mahafali ya 11 tarehe 7, Agosti 2026 ambapo jumla ya wanafunzi 78 wamehitimu masomo yao mwaka huu 2026.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mchungaji Deogratius Msanya, ambaye ni Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, amewataka wahitimu kuongeza juhudi wanapoelekea katika mitihani yao ya mwisho, akifananisha safari yao ya elimu na mbio za marathon.
Mchungaji Msanya amesema wakimbiaji wa mbio ndefu wanapokaribia kufika mwisho wa mbio huongeza nguvu zaidi, hivyo amewataka wahitimu kuongeza bidii katika hatua hii ya mwisho ili wafanye vizuri katika mitihani yao.

Aidha, amewataka wahitimu watakapoingia katika maeneo yao ya kazi kuzingatia maadili ya taaluma zao, akisisitiza kuwa wagonjwa wanahitaji kuoneshwa upendo, utu na heshima. Amewataka pia kuwa makini katika namna wanavyowasiliana na wagonjwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi hiyo, Dkt. Paul Shemdoe, amesema changamoto si kikwazo bali ni fursa ya taasisi kujifunza na kukua. Amezitaja baadhi ya changamoto kuwa ni uchache wa madarasa pamoja na uchakavu wa miundombinu ikiwemo majengo, huku akiomba nguvu ya pamoja katika kuharakisha maendeleo ya taasisi hiyo.

Dkt. Shemdoe ameishukuru Ofisi Kuu ya Dayosisi ya Kaskazini kwa mchango wake mkubwa kwa taasisi hiyo, pamoja na Serikali kwa kuendelea kutoa mwongozo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Mafunzo ya Afya Machame, Prof. Blandina Mbaga, amewataka wahitimu kutambua kuwa taaluma waliyoichagua si lelemama, bali ni taaluma yenye dhamana kubwa inayohitaji maadili na uwajibikaji.

Prof. Mbaga amewataka wahitimu kwenda kazini wakizingatia maadili na kutoa huduma kwa ufanisi, huku akiwakumbusha kutumia teknolojia na akili bandia (AI) kwa uangalifu katika kutafuta taarifa za kitaaluma. Amesisitiza pia umuhimu wa mawasiliano mazuri na wagonjwa, akisema baadhi yao hawaelewi changamoto wanazopitia, hivyo wahitimu wanapaswa kuweka mawasiliano, utu na huduma bora kwa wagonjwa kuwa kipaumbele.