Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Mhandisi Z.S. Moshi, amewakaribisha wageni sita kutoka Ujerumani, ambao ni marafiki wa Usharika wa Shokony, Jimbo la Kilimanjaro Mashariki, waliotembelea Ofisi Kuu ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini leo.
Miongoni mwa wageni hao ni Pastor Dr. Tim Schedel, kutoka Ev.-Luth. Kirchengemeinde Heiligengeist, Kiel, Ujerumani, ambaye ameongoza kundi hilo katika ziara hiyo.
Wageni hao wameambatana na Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki, ambaye pia ni Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Shokony, pamoja na wainjilisti wanne kutoka usharika huo.
Katika ziara hiyo, wageni hao walipata wasilisho kuhusu muhtasari wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, lililotolewa na Bibi Esther Kilimba, IT wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini.
Akitoa wasilisho hilo, Bibi Kilimba alieleza kuhusu Dira, Dhima na Maadili ya Msingi ya Dayosisi, pamoja na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa katika kuimarisha huduma ya Kanisa na maendeleo ya jamii.
Kwa mujibu wa wasilisho hilo, KKKT Dayosisi ya Kaskazini kwa sasa ina jumla ya Sharika 177, wachungaji 244, wainjilisti 443, wadiakonia 131 na Parish Workers 125, pamoja na idadi kubwa ya waumini.
Dayosisi inajihusisha na maeneo mbalimbali ya huduma, yakiwemo umisioni na uinjilisti, huduma za kijamii na kidiaakonia, afya na elimu, uendelevu wa kiuchumi, pamoja na masuala yanayowahusu wanawake, vijana na mazingira.
Ziara hiyo inalenga kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini na marafiki wa Kanisa kutoka Ujerumani, hususan katika kuendeleza huduma na shughuli za Usharika wa Shokony.






