Shule ya watoto wenye ulemavu Faraja Maalum ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini, iliyopo Wilaya ya Siha, Mkoa wa Kilimanjaro imefanya mahafali yake ya 10 ya darasa la saba, huku sherehe hizo zikipambwa na maonesho ya bidhaa zilizobuniwa na wanafunzi wa shule hiyo.
Mahafali hayo yamefanyika tarehe tarehe 11 Septemba, 2026 ambapo Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mchungaji Deogratius Msanya alikuwa mgeni rasmi akimuwakilisha Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Dkt. Frederick Shoo.
Sambamba na Mch.Msanya mahafali hayo yalihudhuriwa na Mke wa Hayati Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Dkt.Erasto Kweka pamoja na Miss. Derby kutoka Faraja Fund Foundation taasisi inayoshirikiana na KKKT Dayosisi ya Kaskazini kufadhili shule ya Faraja Maalumu.
Kabla ya kuanza kwa sherehe hizo na maonesho, wanafunzi wazazi na viongozi wa serikali walioalikwa walifanya ibada ya shukurani ambayo iliambatana na uzinduzi wa vyombo vya muziki katika nyumba ya ibada.
Katika maonesho ya bidhaa mgeni rasmi alipata kusikiliza na kuona ubunifu wa wanafunzi hao katika kutengeneza bidhaa kama vikapu, mikanda, mikoba na nguo.
Katika hotuba yake fupi Mchungaji Msanya amewasisitiza wazazi, walezi na wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana katika kuwasaidia watoto kufikia ndoto zao.
Katika sherehe hizo pia kulikuwa na viongozi wa serikali akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Mhe. Dankan Urassa, ambae alipongeza Kanisa hususani Dayosisi ya Kaskazini kwa mchango wake wa kutoa huduma ya elimu kwa watoto wenye ulemavu wa viungo katika Wilaya ya Siha, akisema Kanisa limechukua jukumu ambalo kwa sehemu lilipaswa kutekelezwa na Serikali.
Mhe.Urassa aliongozana na Afisa Tarafa wa Wilaya ya Siha, Shedrack Mushi, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Siha, aliwapongeza wanafunzi waliohitimu Darasa la Saba pamoja na walimu kwa jitihada walizofanya katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.






