MKUTANO MKUU WA 39 WA KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI WAFANYIKA

Mkutano Mkuu wa 39 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, umefanyika tarehe 20 Agosti 2026 katika viwanja vya Lutheran Uhuru Hotel & Conference Centre, mjini Moshi, Kilimanjaro.

Mkutano huo umefanyika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Katiba ya Dayosisi, inayoeleza kuwa Mkutano Mkuu, ambao ni chombo cha juu zaidi cha maamuzi katika Dayosisi, hufanyika kila baada ya miaka miwili.

Mkutano huo umefanyika wakati Dayosisi ya Kaskazini ikiwa imefikia nusu muhula wa utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Dayosisi wa miaka mitano wa 2024–2028. Umehudhuriwa na washiriki zaidi ya 400, wakiwemo viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali, wajumbe wawakilishi kutoka majimbo yote matano ya Dayosisi ya Kaskazini, viongozi wa serikali pamoja na waalikwa mbalimbali.

Akitoa salamu za kufungua mkutano huo, Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo amegusia nafasi ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini katika kugusa maisha ya binadamu ikiwemo afya, elimu, uchumi, haki za binadamu na utunzaji wa mazingira.

Sambamba na salamu za ufunguzi kutoka kwa Askofu Dkt. Shoo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Godfrey Mnzava, akiwa miongoni mwa waalikwa, ameipongeza Dayosisi ya Kaskazini pamoja na Askofu Dkt. Shoo kwa kuwa mstari wa mbele katika shughuli zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi, ikiwemo utunzaji wa mazingira na utoaji wa huduma za kijamii, mambo ambayo pia ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali.

Neno Kuu la Mkutano

Neno Kuu la Mkutano huo limetoka katika Zaburi 78:3–4:

“Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu, ambayo baba zetu walituambia. Hayo hatutawaficha wana wao, huku tukiwaambia kizazi kingine, sifa za Bwana, na nguvu zake, na mambo yake ya ajabu aliyoyafanya.”

Msomaji wa neno kuu la mkutano, ambaye ni Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dkt. Godson Abel Mollel, ameweka wazi kuwa lengo la neno hilo ni kuwapa wajumbe wa mkutano maarifa ya kujenga familia imara, kisha kupeleka maarifa hayo katika majimbo na sharika zao.

Askofu Dkt. Mollel ameeleza kuwa familia nyingi zinakaa pamoja nyumbani, lakini zikiwa katika mgawanyiko, ambapo kila mwanafamilia huweka umakini katika shughuli yake, kama vile kutumia simu na kutazama vipindi vya televisheni.

Amesema kuna umuhimu wa familia kukaa pamoja, huku wazazi wakijenga utamaduni wa kuwasikiliza watoto na kuwalea kwa mifano bora yenye msingi wa imani, ikiwemo kufanya ibada pamoja.

 Taarifa ya Maendeleo ya Dayosisi

Aidha, taarifa rasmi ya Dayosisi imewasilishwa na Askofu Dkt. Shoo, akielezea maendeleo ya Dayosisi ya Kaskazini katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Dayosisi wa miaka mitano wa 2024–2028.

Ripoti hiyo imegusa maeneo mbalimbali ya vipaumbele vya Mpango Mkakati, ikiwemo ukuaji endelevu wa Kanisa. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kutoka mwezi Septemba 2024 hadi Juni 2026, Dayosisi imekuwa na ongezeko la washarika wapya 27,772.

Akihitimisha Mkutano Mkuu wa 39, Askofu Dkt. Shoo ametoa pongezi kwa wajumbe na waalikwa pamoja na Askofu Dkt. Mollel kwa kushiriki kikamilifu katika mkutano huo.

Aidha, Mkutano Mkuu wa 40, unaotarajiwa kufanyika mwaka 2028, unatarajiwa kuandaliwa na Jimbo la Siha, ambalo liliandaa Mkutano Mkuu wa 35.