Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Dkt. Fredrick Shoo, Mei 17, 2026 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba ya ibada katika Mtaa wa Sayuni, Usharika wa Pumuani Jimbo la Kilimanjaro Mashariki.
Tendo hilo liliambatana na ibada ya kumstaafisha kwa heshima Mch. Lord Macha, iliyofanyika katika Senta ya Usharika wa Pumuani.
Akisoma risala mbele ya Askofu Shoo, Mchungaji kiongozi wa wa Usharika huo, Danstan Meena, alisema waumini wa Mtaa wa Sayuni wenye jumla ya jumuiya tano walikuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufika katika Senta ya Usharika kwa ajili ya ibada.
Alisema hali hiyo ilisababisha baadhi ya waumini kuwa wavivu kushiriki ibada mara kwa mara, jambo lililowasukuma kuanzisha jengo la muda la ibada mwaka 2022 ili kurahisisha huduma za kiroho kwa waumini wa eneo hilo.
Aidha, alisema ujenzi wa jengo jipya la nyumba ya ibada ulianza rasmi Machi 6, 2026, ambapo hadi sasa jumla ya shilingi milioni 27, laki 8 na elfu 50 zimekusanywa kwa ajili ya ujenzi huo.
Mchungaji Meena aliongeza kuwa kukamilika kwa jengo hilo kunatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 515.



