MADAKTARI WA HOSPITALI YA LUTHERANI MARANGU WASHIRIKI MKUTANO MKUBWA WA AFYA TANZANIA

Madaktari kutoka Hospitali ya Lutherani Marangu wameshiriki katika Mkutano wa 13 wa Afya Tanzania (Tanzania Health Summit – THS) 2026, uliofanyika kuanzia Oktoba 5 hadi 7, 2026 Jijini Dar Es Salaam.

Hospitali ya Marangu imewakilishwa na Dkt. Janeth Mgonja na Dkt. Elishadai Kinwasi katika mkutano huo ambao umewakutanisha wataalamu wa afya, watunga sera, washirika wa maendeleo, watafiti na wadau wa jamii kwa ajili ya kujadili mustakabali wa huduma za afya nchini Tanzania na umuhimu wa kujenga mifumo imara ya afya inayoweza kukabiliana na mabadiliko katika mazingira ya kimataifa.

Wawakilishi wa hospitali hiyo wameshiriki katika vikao mbalimbali, ikiwemo vikao vya uwasilishaji wa matokeo ya tafiti na mijadala iliyojikita katika vipaumbele muhimu vya afya.

Masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na kujenga mifumo imara ya afya, afua za VVU na kifua kikuu zinazoongozwa na jamii, huduma za afya ya uzazi na ujinsia, uhuru wa nchi katika kusimamia masuala ya afya, upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, ukusanyaji wa rasilimali za ndani, bima ya afya ya kijamii na ushirikiano endelevu wa kimkakati.

Ujumbe muhimu uliojitokeza katika mkutano huo ni umuhimu wa nchi kumiliki na kusimamia mipango yake ya afya, kuhakikisha uendelevu wa huduma, kuimarisha ushirikiano na kujenga mifumo imara ya afya yenye uwezo wa kukabiliana ipasavyo na mabadiliko ya hali ya afya duniani.

Sambamba na hayo, wameweza kutoa wasilisho katika siku ya mwisho ya mkutano kuhusu mradi wa  Kliniki ya Saratani kwa Njia ya Mtandao (Online Outreach Cancer Clinic – OOCC),yenye  mada isemayo “Kuanzia Ugunduzi wa Saratani hadi Matibabu” (From Cancer Detection to Treatment).

Uwasilishaji huo umeeleza uzoefu na mafunzo yaliyopatikana kupitia ushirikiano wa OOCC kati ya Hospitali ya Lutherani Marangu, Kituo cha Afya cha Africa Amini Alama kilichopo Arusha, na Kliniki ya Urban Care iliyopo Zanzibar.

Ushirikiano huo umeonesha namna teknolojia ya kidijitali katika huduma za afya, ushirikiano wa wataalamu kutoka taaluma mbalimbali na ubia wa kimkakati vinavyoweza kusaidia kupunguza mapungufu katika huduma za saratani, kuimarisha mifumo ya rufaa na kuboresha upatikanaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani kwa wakati.

Hospitali ya Lutherani Marangu inaendelea kujizatiti katika kujifunza, ubunifu, ushirikiano na kuimarisha mahusiano na washirika mbalimbali ili kuchangia upatikanaji wa huduma za afya zilizo bora, zinazopatikana kwa urahisi, zinazotolewa kwa usawa na zenye uendelevu nchini Tanzania.