KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Jimbo la Hai, limezindua rasmi kampeni ya “Hai ya Kijani”, inayolenga kupanda miti 20,000 katika sharika na vituo mbalimbali vya jimbo hilo ifikapo mwishoni mwa mwaka 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda mazingira na kuhamasisha jamii kushiriki katika upandaji na utunzaji wa miti.
Uzinduzi huo umefanyika, Oktoba 27, 2026, katika Ofisi Kuu za Jimbo la Hai, ukiongozwa na Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Dkt. Fredrick Shoo, na kushirikisha viongozi wa Kanisa, maafisa wa serikali pamoja na wadau wa utunzaji wa mazingira. Akizungumza katika uzinduzi huo, Askofu Shoo ameonesha kukerwa na viongozi na wananchi wanaoharibu mazingira kwa manufaa binafsi, akionya kuwa vitendo hivyo, ikiwemo ukataji wa miti, vinahatarisha maisha ya viumbe na mustakabali wa ulimwengu.
Amesisitiza kuwa miti ni mapafu ya ulimwengu, akieleza kuwa kutunza mazingira ni kutunza uhai na kwamba juhudi za kuyahifadhi zinapaswa kuzingatia mahitaji ya kizazi cha sasa na kijacho. Askofu Shoo ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendeleza utunzaji wa mazingira, kabla ya kuzindua rasmi kampeni hiyo kwa kupanda mti. Kampeni ya Hai ya Kijani imeratibiwa kwa ushirikiano kati ya KKKT Jimbo la Hai na Shirika Lisilo la Kiserikali la Kijani Pamoja, ikiwa na lengo la kuhamasisha na kutekeleza upandaji wa miti katika sharika mbalimbali za jimbo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa KKKT Jimbo la Hai, Mchungaji Biniel Mallyo, amesema jimbo hilo linajivunia kampeni hiyo, akieleza kuwa utunzaji wa mazingira ni sehemu ya wajibu ambao Mungu amewapa wanadamu. Naye Lukiko Balagaza kutoka Shirika la Kijani Pamoja ameeleza umuhimu wa kupanda miti katika kupunguza hewa chafu na kuboresha upatikanaji wa hewa safi, huku Mateso Mtangazo kutoka Idara ya Maliasili ya Wilaya ya Hai akitoa maelekezo ya kitaalamu kuhusu namna sahihi ya kupanda na kuitunza miti ili kuhakikisha inastawi.
Aidha, Matatizo, Tangazo Afisa Mazingira kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Hai, ametoa shukrani kwa Askofu Shoo kwa kukemea uharibifu wa mazingira, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuhamasisha jamii kuhusu uhifadhi wa mazingira. Katika kuimarisha ushirikiano wa taasisi za kidini katika juhudi hizo, Mchungaji Emmanuel Michael kutoka Kanisa la Anglikana Hai ameahidi kuendeleza ushirikiano baina ya makanisa kwa lengo la kuokoa mazingira. Kampeni ya Hai ya Kijani inalenga kuifanya jamii kuwa sehemu ya juhudi za upandaji na utunzaji wa miti, kwa matumaini ya kulinda mazingira na kujenga mazingira bora kwa vizazi vijavyo.






