Matendo makuu manne yamekuwa kiini cha ibada iliyoongozwa na Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, katika Chuo cha Biblia na Theolojia Mwika, yakihusisha kustaafu kwa heshima kwa mtumishi wa Kanisa, maadhimisho ya miaka 50 ya uhusiano wa kimataifa, miaka 25 ya kozi ya Theolojia na mahafali ya 73 ya chuo hicho.
Matendo hayo ni pamoja na kustaafishwa kwa heshima kwa Mchungaji Dkt. Emilian Ndosi, aliyekuwa mkufunzi wa Chuo cha Biblia na Theolojia Mwika; kuadhimisha miaka 50 ya uhusiano kati ya Jimbo la Weiden la Kanisa la Kilutheri la Bavaria nchini Ujerumani na chuo hicho; kuadhimisha miaka 25 ya wahitimu wa Theolojia tangu kuanza kwa kozi hiyo mwaka 2001; pamoja na kuongoza mahafali ya 73 ya chuo hicho.
Akizungumza katika ibada hiyo, Askofu Shoo amesema mafunzo yanayotolewa katika chuo hicho ni bora na yanawaandaa watumishi wazuri wa Kanisa, akisisitiza kuwa ubora huo ni sifa kwa Mungu na unapaswa kuendelea kuwa alama ya chuo hicho. Aliwataka wahitimu kuzingatia uaminifu, uvumilivu na kujitoa katika kumtumikia Mungu, akiwahimiza kutekeleza majukumu yao kwa bidii na uaminifu katika maeneo watakayopangiwa kutumikia.
Askofu Shoo aliwashukuru wageni kutoka Jimbo la Weiden nchini Ujerumani kwa kushiriki maadhimisho hayo, akieleza kuwa utamaduni wa kutembeleana unaimarisha uhusiano kati ya taasisi na watu. Alisema uhusiano wa kweli hujengwa pale watu wanapokutana ana kwa ana, akibainisha kuwa uwepo wa wageni hao katika maadhimisho hayo ni kielelezo cha ushirikiano ulioimarika kati yao na Chuo cha Biblia na Theolojia Mwika.
Vilevile, aliwashukuru kwa kushiriki kuchangia ujenzi wa hosteli ya wanawake chuoni hapo, huku akiwahimiza kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya chuo na huduma ya Kanisa. Akihitimisha hotuba yake, Askofu Shoo alimpongeza Mchungaji kwa hatua ya Kustaafu pamoja na wahitimu ambapo aliwakumbusha wahitimu hao kuwa kuhitimu kwao ni mwanzo wa hatua nyingine ya utumishi, akiwataka kwenda kupigana vita vyema vya imani kwa uaminifu na bidii.
Katika mahafali hayo, wahitimu walihusishwa na programu mbalimbali za mafunzo, zikiwemo Astashahada ya Elimu ya Kikristo na Uinjilisti, Astashahada ya Wasaidizi wa Sharika na Huduma za Jamii, pamoja na Astashahada na Stashahada ya Muziki wa Kanisa.Matukio hayo manne yameifanya Oktoba 24, 2026 kuwa siku ya kihistoria kwa Chuo cha Biblia na Theolojia Mwika, ikikutanisha heshima kwa watumishi wa Kanisa, kuimarisha uhusiano wa kimataifa, kuadhimisha hatua muhimu za kielimu.







