Kwaya 32 zashiriki Sikukuu ya uimbaji KKKT Dayosisi ya Kaskazini mwaka 2026, huku ujumbe wa msingi ukielekezwa katika kuzingatia uimbaji wa kimatengenezo na kuzingatia kuwa sikukuu hiyo si mashindano bali ni tukio la kumuimbia Mungu.
Sikukuu hiyo imeadhimishwa siku ya Jumapili Oktoba 25,2026 katika usharika wa Nshara, Jimbo la Hai.
Katika mahubiri yake wakati wa ibada iliyotangulia kabla ya uimbaji Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Mchungaji Deogratius Msanya, amesema kuwa ujumbe wa Siku Kuu ya Uimbaji Dayosisi na Siku ya Matengenezo ya Kanisa ni wito wa kumwimbia Bwana, ambaye ni Mwamba wa wokovu wetu. Amesisitiza kuwa tunaokolewa kwa neema, kama alivyofundisha Martin Luther wakati wa Matengenezo ya Kanisa.
Amesema kuwa tunaitwa kumwimbia Mungu kwa sababu yeye ndiye Mwamba wa wokovu wetu. Kwa mujibu wake, wito wa kumwimbia Mungu una uhusiano mkubwa na Matengenezo ya Kanisa, kwani wokovu haupatikani kwa kununuliwa kwa fedha, bali ni kwa neema ya Mungu. Hiyo ndiyo sababu tunamwimbia Bwana, Mwamba wa wokovu wetu.
Mchungaji Msanya amewataka waimbaji kutafakari huduma yao kwa mtazamo wa Matengenezo ya Kanisa. Amesisitiza kuwa uimbaji haupaswi kumtukuza mwanadamu yeyote, bali Kristo pekee. Amesema hatarajii kuona waimbaji wakinuniana baada ya uimbaji au baada ya matokeo kutangazwa, isipokuwa pale ambapo mtu anaimba kwa lengo la kujitukuza mwenyewe badala ya kumtukuza Kristo.
“Tukumbuke kuwa kupigiwa makofi kunaweza kuisha, nafasi yako inaweza kusahaulika na jina lako pia linaweza kusahaulika, lakini Mungu hataisahau kazi yako njema,” amesisitiza. Aidha, amewapongeza waimbaji kwa kutenga muda wao kwa ajili ya mazoezi ya kwaya, akiwahakikishia kuwa Mungu si dhalimu hataisahau kazi yao.
Amesisitiza kuwa tunatambua wokovu kwa neema, tunaishi kwa neema na vipawa vyetu vyote ni kwa neema. Akirejelea mafundisho ya Martin Luther, amekumbusha kuwa wokovu haupatikani kwa kununua vyeti vya msamaha, bali ni kwa neema ya Mungu.
“Hakuna haja ya kujivunia kipawa cha aina yoyote, kwa sababu vyote ni kwa neema ya Mungu,” amesisitiza. Huduma ya uimbaji inahitaji mioyo iliyopondeka. Amesema kuwa huduma ya uimbaji inahitaji sauti nzuri zilizopangiliwa kitaalamu, lakini jambo la msingi zaidi ni kuwa na mioyo iliyopondeka mbele za Mungu.
Ameonya kuwa waimbaji wanapopongezwa kwa huduma yao, hawapaswi kujisifu kwa kusema kuwa mafanikio yao yametokana na juhudi zao pekee, ikiwemo kuamka usiku kufanya mazoezi, kwa sababu kufanya hivyo ni kuchukua utukufu unaomstahili Mungu. Vilevile, amesema kuwa kwaya inapopata alama nzuri na kisha kusema kuwa haikuwa katika ubora wake, inapaswa kutafakari kama kauli hiyo inaashiria kushindwa kutambua neema ya Mungu katika mafanikio yao.






