Askofu Andreas Holmberg kutoka Kanisa la Sweden, Dayosisi ya Stockholm, pamoja na mkewe Mch. Cecilia, wameshiriki sala ya asubuhi katika Makao Makuu ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, leo Novemba 24, 2026.
Akitoa salamu katika ibada hiyo, Askofu Holmberg amewasalimu watumishi wa ofisi kuu na kueleza furaha yake ya kurejea tena Dayosisi ya Kaskazini, huku akibainisha kuwa katika siku mbili tangu alipowasili, amepata fursa ya kutembelea vituo mbalimbali vya Dayosisi hiyo.
Kwa upande wake, Mch. Cecilia ameeleza furaha yake ya kurejea Dayosisi ya Kaskazini baada ya miaka 21 tangu alipoondoka mjini Moshi, ambako aliwahi kuishi na kutumika.Sambamba na salamu hizo, Askofu Holmberg amekabidhi zawadi kwa ofisi kuu ya Dayosisi kama ishara ya kuendeleza ushirikiano na uhusiano wa muda mrefu baina ya Dayosisi ya Stockholm na Dayosisi ya Kaskazini, ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 10.
Akizungumza kwa niaba ya ofisi kuu ya Dayosisi ya Kaskazini, Katibu Mkuu Msaidizi, Bw. Christian Philipo, amemshukuru Askofu Holmberg na mkewe kwa ujio wao pamoja na zawadi walizokabidhi, akisema Dayosisi inathamini upendo na moyo wa ushirikiano ambao wameendelea kuuonesha.
“Tunashukuru kwa upendo na mapenzi mema ambayo mmeendelea kutuonesha sisi Dayosisi ya Kaskazini. Tumeyaona katika matukio mengi, lakini pia katika namna ambavyo mmeendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Sweden, hususan Dayosisi ya Stockholm, na sisi Dayosisi ya Kaskazini. Alama hizi mnazoendelea kuziweka katikati yetu, zikiambatana na upendo mnaotuonesha kwa moyo, zitaendelea kudumu milele,” amesema Bw. Philipo.
Askofu Holmberg na mkewe waliwahi kuishi na kutumika nchini Tanzania mwanzoni mwa miaka ya 2000. Katika kipindi hicho, Askofu Holmberg alikuwa mwalimu wa Theolojia katika Chuo cha Biblia na Theolojia Mwika, kilicho chini ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini, huku mkewe, Mch. Cecilia, akihudumu kama mchungaji wa vijana.
Ujio wao unafuatia ziara ya ujumbe wa watu 16 kutoka Dayosisi ya Stockholm, uliofanya ziara katika maeneo mbalimbali ya Dayosisi ya Kaskazini siku chache zilizopita.Ziara hizo zinaendelea kudhihirisha kuimarika kwa uhusiano na ushirikiano kati ya Dayosisi hizi mbili, zinazounganishwa na umoja wa imani na dhamira ya pamoja ya kuujenga mwili wa Yesu Kristo.

