Askofu Dkt. Shoo achaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Baraza la Makanisa Duniani (WCC)

Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, amechaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Baraza la Makanisa Duniani (WCC) katika Mkutano wa 11 wa baraza hilo uliofanyika  nchini Ujerumani kuanzia Agosti 29 hadi Septemba 8, 2022.  Mkutano huo hufanyika mara moja takribani kila baada ya miaka 7.

Askofu Dkt. Shoo licha ya kuwa Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini, pia ndiye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania Tanzania (CCT) yenye Makanisa wanachama 12 na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Makanisa ya Kilutheri ya Afrika Mashariki na Kati yenye Makanisa Waanachama toka nchi 8 za Tanzania, Uganda, Kongo (DRC), Kenya, Rwanda, Madagascar, Ethiopia na Eritrea.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni (WCC) ni ushirika wa Makanisa yanayomkiri Bwana Yesu Kristo kuwa Bwana  na Mwokozi kulingana na maandiko matakatifu yanavyofundisha na linatimiza wito wao wa pamoja kwa utukufu wa Mungu mmoja, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

WCC ilianzishwa mwaka 1948 na ina Makanisa Wanachama 352 yenye waumini zaidi ya milioni 580 kutoka madhehebu ya Anglican, Lutheran, Methodist, Baptist, Katoliki na mengine katika nchi 120.

Viongozi wengine hapa nchini ambao wamewahi kushika wadhifa huo ni Askofu Dkt. Alex Malasusa na Askofu Dkt. Owdenburg Mdegella.