Askofu Dkt. Shoo afungua Easter Conference Mkoa wa Kilimanjaro; Zaidi ya Vijana 880 wahudhuria

Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, amefungua Juma la  Maburudisho ya Pasaka (Easter Conference) la Ushirika wa Wanafunzi wa Kikristo Tanzania (UKWATA) Mkoa wa Kilimanjaro  Aprili 7, 2023 katika chuo cha Biblia na Theologia Mwika.

Zaidi ya vijana 880 kutoka Makanisa yliyopo chini ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) wamehudhuria Maburudisho hayo ya siku 4.

Akihubiri katika Ibada hiyo ambayo ni siku ya Ijumaa Kuu, Baba Askofu Shoo alisema Ijumaa kuu ni siku ya kutafakari upendo wa Mungu wa kumtoa mwana wake wa pekee ili mwanadamu apate kuokolewa.

Alisema kijana Mkristo anapaswa kutambua kuwa wokovu ni mpango wa Mungu kwa watu wote na kila aliitiaye jina la Bwana ataokolewa.

“Nikwambie Kijana Mkristo jisikie uko salama mikononi mwa Yesu Kristo, tembea kwa amani ukijua Yesu aliyeshinda mauti naye atakushindia hata pale unapopita katika shida na mateso”. Alisema Askofu Dkt. Shoo

Aidha, aliwatahadharisha vijana kuacha kuiga mambo yasiyofaa kama ushoga, usagaji, ulawiti n.k kwa sababu tu, yametambulishwa na wale watu maarufu. “Niwaombe msishawishike na hata kama umejaribiwa kuingia huko kama upo hapa kataa kwa jina la Yesu”.Alisema

Alisema suala la ushoga, usagaji na ndoa za jinsia moja ni kusudi la shetani na haukuwa mpango wa Mungu. Kanisa limepinga ndoa za jinsia moja mara zote hata kutoa matamko kadhaa kuanzia na tamko la mwaka 2004 lakupinga ndoa za jinsia moja. Aliwataka vijana kupinga kwa nguvu zote yale yote yanayokwenda kinyume na mpango wa Mungu wa uumbaji.

Alisema tunapaswa kuacha kushabikia mambo ambayo hayakumpendeza Mungu maana ni machukizo mbele za Mungu na kunukuu maneno ya Biblia kutoka kitabu cha Mambo ya Walawi 20:13 ‘Tena mwanamume akilala pamoja na mwanamume, kama alalavyo na mwanamke, wote wawili wamefanya machukizo; hakika watauawa; damu yao itakuwa juu yao.

Anasema matendo maovu yanamfanya Mungu kumuacha mwanadamu afanye anavyotaka na Mungu akituacha, akimwacha mwandamu na taifa matokeo yake ndiyo haya tunayoyaona ya mambo yasiyofaa.

‘Kwa hiyo, Mungu aliwaachia wafuate tamaa zao za aibu. Hata wanawake wao waliacha matumizi ya asili ya maumbile yao wakatumia miili yao isivyokusudiwa. Hali kadhalika wanaume waliacha uhusiano wa asili kati ya waume na wake wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume walifanyiana mambo ya aibu, nao waka pata katika miili yao adhabu waliyostahili kama matokeo ya uovu wao’ Alinukuu Maneno hayo kutoka kitabu cha Warumi 1:26&27 akionyesha athari za kuachwa na Mungu kwa sababu ya Maovu ya Wanadamu.

Alihitimisha kwa kuwaasa vijana Wakristo kutunza na kuhifadhi miili yao maana mwili ni hekalu la Mungu.

Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo mwenye fimbo, Mkuu wa Jimbo la K/Masharki wa pili kushoto, kwenye picha ya pamoja na waalimu, wachungaji, wenzi wa wachungaji na wanafunzi wa UKWATA baada ya ufunguzi wa Easter Conference Aprili 7, 2023