Askofu Dkt. Shoo Afungua Kanisa Siha Sango

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (Mstaafu) ambaye ni Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, amefungua na kuweka wakfu Kanisa jipya la Usharika wa Siha Sango la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Jimbo la Siha Machi 10, 2024.

Ujenzi wa Kanisa hilo ulianza mwaka 2001 na hadi kukamilika umegharimu kiasi cha shilingi za Kitanzania zaidi ya milioni 455, fedha ambazo ni michango ya Washarika wa Siha Sango waliopo ndani na nje ya Usharika pamoja na marafiki.

Kwa mujibu wa risala iliyosomwa usharikani hapo, mwaka 1899 kilianzishwa kituo Cha misioni Siha. Wakristo wa kwanza mwaka 1940 waliabudu kwenye jengo la miti na jengo la kudumu lilianza kujengwa mwaka 1941 na kukamilika mwaka 1945 Mangi Gidion akiwa mwenyekiti wa ujenzi huo.

Inaelezwa kuwa matofali yalichongwa katika mwamba wa bonde na mlima wa Moramu unaoitwa Nshuhui katika kijiji cha Kishisha kitongoji cha Nshuhui takribani kilomita mbili na nusu kufika Siha Sango na aliyeweza kubeba jiwe moja alipewa likizo ya wiki mbili bila kushiriki kazi za utawala.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Askofu Dkt. Shoo awali aliwapongeza washarika wa Siha Sango kwa kazi kubwa waliyofanya ya kumjengea Mungu nyumba nzuri ya Ibada.

Alisema kazi hii inadhihirisha Imani yao kubwa waliyorithishwa na wamisionari waliofika hapo na kuanzisha kituo cha misioni mwaka1899. Wazazi wenu walirithishwa Imani na wamisionari na wao wakaishika na kuirithisha kwenu.

Alisema kazi waliyoifanya ni itikio la Imani na ushuhuda wao kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

“Ndugu zangu nawaombeni, kwakuwa nyumba hii imekamilika na imewekwa wakfu muiitumie kwa ibada kwa kujifunza neno la Mungu kama mnataka amani ya kweli maana Amani ya kweli inapatikana kwa Mungui” Alisema Askofu Dkt. Shoo.

Faraja Maalumu Wazindua Albamu

Katika ibada hiyo sambamba na ufunguzi wa Kanisa, Askofu Dkt. Shoo alizindua albamu ya 4 walioyoipa jina la Tazama Ulivyoniumba ya kwaya ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya watoto wenye ulemavu wa viungo Faraja maalum ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini iliyopo Sanya Juu Sabuko.

Akizindua albamu hiyo, Askofu Dkt. Shoo alisema watoto wa Faraja pamoja na ulemavu wao wa viungo lakini wamefanya mambo mazuri ikiwemo kumtumikia Mungu kwa njia ya nyimbo.

“Niwaambie kwamba watoto hawa ni walemavu wa viungo lakini si walemavu katika vichwa vyao. Shule hii imekuwa miongini mwa shule zinazoongoza kiwilaya katika mitihani ya Taifa. Angalia wanamwimbia Bwana wanatoa ushuhuda, tuwatie moyo waendelee kumtukuza Mungu ambaye Mungu ndiye furaha ya mioyo yao” Alisema Askofu Dkt. Shoo.

Askofu Dkt. Fredrick Shoo Akikata Utepe Kuzindua Kanisa Jipya KKKT Sia Sango