Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo ametoa rai kwa watu wote kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi litakalofanyika Agosti 23, 2022 nchini Tanzania.
Anasema zoezi la sensa ni la muhimu katika nchi na ni utaratibu wa serekali zote Duniani kujua idadi ya watu na hali ya watu wake ili kuweza kupanga huduma na mipango ya maendeleo ya jamii.
Askofu shoo alitoa rai hiyo katika Ibada ya kuwabariki wanafunzi wa Udiakonia katika kituo cha mafunzo ya Udiakonia Faraja Sanya Juu jimbo la Siha la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Jumapili Agosti 21, 2022.
Aliwapongeza na kuwatakia Baraka za Mungu wahitimu hao akiwataka kuimarisha Ushirika huo.
Kadhalika aliwataka wahitimu hao kutambua wito wao na kumtambua aliyewaita na kusudi la kuwaita katika kumtumikia.
Amesema wameitwa kuwatumikia watu wa Mungu kwa neno na kwa tendo na kueleza kuwa udiakonia unajidhihirisha kwa matendo ya huruma hivyo wanapaswa kuwa mstari wa mbele kutafsiri Injili ya Yesu Kristo na upendo wa Mungu katika matendo ya huruma na Upendo.
“Muwapende watu wa Mungu ambao mnatumwa kuwahudumia na mkaipndende sana hudumahii mkifanya kazi kwa bidi kama mtume Paulo anavyosema alifanya kazi usiku na mchana bila kujihurumia na kulinda uadilifu na maadili ya kazi aliyoitiwa”. Alisema Dkt. Shoo.
Aidha aliwataka kufanya kazi kwa bidii bila kutanguliza maslahi binafsi kwa kutaka kujitajirisha kwa haraka na kusahau huduma waliyoitiwa.
Jumla ya wadiakonia 14 walibarikiwa kwa mujibu wa Kaka Mkuu Mdiakonia Gudluck Nko.