Askofu Dkt. Shoo: Bodi na Kamati simamieni vituo mlivyokabidhiwa

Mkuu wa Kanisa na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo amezitaka bodi na kamati za shule na vyuo kusimamia vituo walivyokabidhiwa kwa niaba ya Dayosisi kuhakisha wanatekeleza mipango na madhumuni yaliyowekwa. Askofu Shoo aliyasema hayo kwenye semina ya wakuu wa shule, wajumbe wa bodi na kamati za shule na vyuo vya Dayosisi iliyofanyika Aprili 21, 2022 Umoja Hosteli.

Askofu Shoo alisema bodi na kamati zinawajibu wa kusimamia vituo walivyokabidhiwa na Dayosisi katika kutimiza sera, madhumuni na miongozo iliyowekwa. “Bodi na Kamati nyie mnamuwakilisha mteuzi wenu ambaye ni Dayosisi katika kusimamia na kutoa taarifa za maendeleo ya vituo mlivyokabidhiwa.”Alisema Dkt. Shoo

Pia aliwataka wenyeviti wa Bodi kuwa na mahusiano na mawasiliano ya mara kwa mara na uongozi wa Dayosisi kujadili na kutoa taarifa ya maendeleo ya vituo wanavyovisimamia kwa kuwa wao ndiyo jicho na sikio la Dayosisi.

Naye Katibu Mkuu wa Dayosisi Mhandisi Zebhadia Moshi katika mada yake ya Utawala Bora alitaja wajibu wa Bodi katika taasisi kuwa ni pamoja na kuwajibika kwa mamlaka ya uteuzi mbayo ni Dayosisi, kusimamia taasisi waliyokabidhiwa kulingana na madhumuni, sheria, sera na miongozo iliyowekwa.

Mhandisi Moshi alisema Bodi inapaswa kuwa msimamizi pekee na sio mtendaji wala  mwendeshaji wa taasisi.

Katika mada hiyo alifafanua kuwa utawala bora unamisingi yake ambayo ni nidhamu (Discipline), uongozi wenye uwezo (leadership competency) na uwajibikaji (accountability).

Katika hatua nyingine Mkuu wa Kanisa na Dayosisi Askofu Dkt. Shoo aligawa zawadi kwa shule zilizofanya vizuri na wanafunzi waliopata alama za juu katika mitihani ya kidato cha nne na sita.

Katibu wa Elimu Dkt. Estomihi Makyara alitaja shule iliyoongoza katika mitihani ya kidato cha nne kwa mwakaa 2021 kwa shule za Dayosisi kuwa ni Agape Junior Seminary ikifuatiwa na Natiro iliyoonyesha mjengio chanya kati ya shule sita za Dayosisi.

Kwa upande wa kidato cha sita shule ya sekondari Msufini iliongoza ikifuatiwa na sekondari  ya Uroki ambayo nayo imeonyesha mjengio chanya katika ufaulu huku shule ya msingi Benjamini Moshi ikiongoza kwa ufaulu kwa shule za Msingi na kufuatiwa na Masama English Medium.

Zawadi zilizotolewa kwa shule zilizofanya vizuri ni kompyuta mpakato, cheti na kombe (trophy). Kwa wanafunzi waliofanya vizuri walizawadiwa cheti cha pongezi, fedha na ipad.